Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO limetoa taarifa likilaani shambulio la utekaji nyara lililotekelezwa siku ya Jumapili na magaidi dhidi ya kanisa la Our Lady of Salvation huko katika mji wa Baghdad nchini Iraq.
Taarifa hiyo ya Isesco imesema kuwa kitendo hicho cha kigaidi ni jinai ya kuaibisha na kwamba dini ya Kiislamu inalaani vikali vitendo kama hivyo. Imeongeza kwamba watu waliohusika na kitendo hicho cha kuaibisha wanapaswa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili waadhibiwe.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba umwagaji damu usiohalalishwa ni jambo linalolaaniwa na kuharamishwa na Uislamu.
Taarifa hiyo imesema mwishoni kuwa kila aina ya shambulio dhidi ya maeneo ya ibada, yawe ni makanisa au misikiti, ni kitendo cha jinai kinachopaswa kukemewa kwa sababu kinakwenda kinyume na utu wa mwanadamu. Makumi ya watu akiwemo kasisi wa kanisa hilo waliuawa katika tukio la kutekwa nyara na kukombolewa mateka wa tukio hilo la kigaidi. 687852