IQNA

Pakistan yaadhimisha siku ya kuzaliwa Iqbal Lahori

13:19 - November 10, 2010
Habari ID: 2029425
Wananchi wa Pakistan jana waliadhimisha mwaka wa 133 tangu kuzaliwa mshairi, mwanafalsafa na mwanafikra wa Kiislamu Allama Muhammad Iqbal Lahori. Sherehe kama hizo pia zimefanyika katika jimbo la Kashmir.
Sherehe hizo ziliambatana na dua makhsusi kwa ajili ya umoja na mafanikio ya taifa la Pakistan na ustawi wa Waislamu kote duniani. Vilevile kiraa ya al Fatiha ilisomwa katika misikiti ya Pakistan.
Serikali ya Pakistan imetangaza siku ya kumbukumbu ya Allama Iqbal kuwa na siku ya mapumziko ili kufanikisha maadhimisho yake.
Maonyesho ya vitabu vilivyoandikwa na mwanafikra huyo wa Kiislamu pia yamefanyika katika Jumba la Makumbusho la Iqbal mjini Lahore, Jumba la Makumbusho la Taifa la Pakistan mjini Karachi na nyumbani kwa marehemu Iqbal.
Vyombo vya habari vya Pakistan, vituo vya utamaduni na jumuiya mbalimbali zimeadhimisha siku hiyo kwa ratiba na vipindi maalumu.
Allama Muhammad Iqbal Lahori alizaliwa tarehe 9 Novemba 1877 katika mji wa Sialkot na alifariki dunia Aprili 21 mwaka 1938 akiwa na umri wa miaka 60. Alianza kuwazindua Waislamu wa bara Hindi kupitia mashairi na kuwahimiza kuunda nchi yao huru ili waweze kuishi kwa izza na heshima na kudhamini haki zao za kijamii, kisiasa na kidini. Alikuwa miongoni mwa wanafikra waliotilia mkazo mno suala la kuhuisha utawala wa kisiasa, kidini na kiroho wa Kiislamu. Iqbal alikuwa na mchango mkubwa katika kuwahimiza Waislamu wa India kuanzisha dola huru la Waislamu huko kaskazini magharibi mwa India yaani Pakistan ya sasa. 692325

captcha