Hayo yamedokezwa katika kikao cha waandishi habari kuhusu Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu kilichofanyika Januari mosi mjini Tehran katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ya Iran. Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Jihadi ya Vyuo Vikuu Muhammad Hussein Yadegari, Hujjatul Islam Naseri mkuu wa mkoa wa Khorassan Razavi (mkoa mwenyeji wa mashindano) na katibu wa mashindano hayo.
Yadegari amesema lengo la mashindano hayo ya Qur'ani ni kuimarisha umoja wa wanachuo Waislamu, kustawisha mawasiliano ya kisayansi kati ya wasomi bingwa wa ulimwengu wa Kiislamu na kuwahimiza wanachuo na wasomi wa vyuo vikuu kushiriki katika masuala ya Qur'ani. Amesema kushiriki wanachuo Waislamu kutoka maeneo yote duniani katika mashindano ya Qur'ani nchini Iran ni fursa ya kuimarisha Umoja wa Kiislamu.
Aidha ameashiria mipango ya Jumuiya ya Shughuli za Qur'ani ya Wanachuo wa Iran –ISQAO- ambayo inafungamana na Jumuiya ya Jihadi ya Vyuo Vikuu na kusema ISQAO inalenga zaidi masuala ya utafiti.
Kwingineko katika kikao hicho na waandishi habari, Hujjatul Islam Nasseri amezungumza kuhusu maandalizi ya mashindano hayo na kusema matayarisho yamekuwa yakiendelea kwa muda wa miezi sita.
722593