Sayyid Muhammad Baqir an-Nassir, mwanafikra wa Kishia wa Saudi Arabia ambaye pia ni hatibu wa swala ya Ijumaa ya mji wa al-Khubar amekosoa vikali kuendelea kuzuiwa Mashia wa nchi hiyo kutekeleza swala za jamaa na kusema kuwa marufuku hiyo ni dhulma kubwa kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Sayyid Muhammad Baqir an-Nassir amesema kuwa ombi la Mashia la kuswali swala za jamaa si upinzani wa kisiasa. Taraifa iliyotolewa na sheikh huyo inasema kuwa mwanazuoni huyo amekamatwa mara kadhaa na askari usalama wa Saudia na kushurutishwa achague baina ya kutoswali swala ya jamaa au afungwe jela. Amesema lengo lake la kutoa taarifa hiyo ni kufikisha sauti na malalamiko ya Mashia kwa viongozi wa serikali na wala sio propaganda kama baadhi ya watu wenye chuki serikalini wanavyojaribu kuonyesha.
Amesema kuna baadhi ya viongozi wa kieneo wanaojaribu kutumia vibaya marufuku ya Mashia kuswali swala za jamaa na kwamba wanatayarisha ripoti za uongo kuhusu jambo hilo ili kuchochea mgawanyiko na chuki kati ya serikali na wakazi wa Khubar, jambo ambalo amesema limepelekea kudhulumiwa zaidi Mashia.
Amelaani vikali marufuku hiyo na kuhoji ni kwa nini misikiti ya Mashia inafungwa ilihali Waislamu wengine wanapewa uhuru kamili wa kuabudu na kutekeleza ibada zao bila vizuizi vyovyote? Ameuliza, ni kwa nini vyombo vya usalama vya Saudia vinatoa idhini ya Mashia kudhulumiwa kwa kiwango hicho? Amemwomba Mwenyezi Mungu adhamini usalama, uthabiti na umoja wa nchi za Kiislamu na Waislamu.
Tunakumbusha hapa kwamba Mashia wa Saudi Arabia ambao wanaunda zaidi ya asimilia 15 ya jamii ya nchi hiyo wanakabiliwa na mashinikizo makubwa ya kiusalama kutoka kwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo na licha ya kuwa misikiti yao imefungwa kutokana na visingizio visivyo na msingi, wakazi wa Khubar hawana ruhusa ya kuswali swala za jamaa katika mji huo. 726496