Sherehe za ufunguzi wa mashindano hayo zimefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa IRIB na kuhudhuriwa na maafisa waandamizi wa masuala ya Qur'ani na Utamaduni nchini Iran pamoja na wananchi wa matabaka mbalimbali.
Sherehe hizo zimefunguliwa kwa kisomo cha Qur'ani Tukufu cha karii Muhammad Hassan Muwahhidi aliyechukua nafasi ya kwanza katika mashindano yaliyopita.
Baada ya hapo Gavana wa Mkoa wa Khurasan Razavi Mahmoud Salahi alitoa hotuba ya kuwakaribisha washiriki na kusema kuwa ni fahari yake kuwa mwenyeji wa makarii na mahafidh wa Qur'ani Tukufu.
“Ni furaha kubwa kuwa Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu yanafanyika katika Mash'had-ur-Riza –AS- yaani mji mtakatifu wa Mash'had ambao mwaka jana ulitangazwa kuwa mji mkuu wa masuala ya kiroho wa Iran”, amesema.
Bw. Salahi pia amesoma ujumbe wa Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashindano hayo. Katika ujumbe wake Rais Ahmadinejad amesisitiza kuwa Qur'ani ni kitabu cha muongozo, nuru na tiba.
Aidha ujumbe wa Ayatullah Nasser Makarem Shirazi umesomwa katika sherehe hizo. Katika ujumbe wake Ayatullah Makarem Shirazi ambaye ni marjaa taqlidi amesema kuhifadhi na kusoma aya za Qur'ani ni amali njema lakini amewataka washiriki wasisahau kuwa, kwa msingi wa aya ya 29 ya suratu Swad inayosema: “Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie aya zake, na wawaidhike wenye akili”, lengo kuu ni kutafakari na kuzingatia aya za Qur'ani Tukufu na kutekeleza maamrisho yake.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Jihad ya Vyuo Vikuu Muhammad Hussein Yadegari amesema kuwa mashindano hayo ya kimataifa ya Qur'ani yana baraka maalumu kitaifa na kimataifa. Ameongeza kuwa mashindano hayo yameleta harakati kubwa ya Qur'ani nchini Iran hasa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Mkurugenzi wa Shirika la Kiislamu la Elimu, Sayansi na Utamaduni ISESCO Dkt. Abdulazizi Othman Altwaijri pia ametuma ujumbe katika mashindano hayo. Katika ujumbe wake mkuu wa ISESCO ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuandaa mashindano hayo na ametoa wito kwa nchi zingine za Kiislamu kutoa mchango wao katika kuinia kiwango cha mashindano hayo ya Qur'ani. Akizungumza katika sherehe hizo za ufunguzi Hujjatul Islam Hamid Muhammadi Naibu Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Iran anayeshughulikia masuala ya Qur'ani amesisitiza kuwa kusoma na kuhifadhi Qur'ani ni mwanzo wa kutekelezwa mafundisho ya Kitabu Kitakatifu. Ametoa wito kwa Waislamu kulipa kipaumbele suala la umoja wa Kiislamu ambao umesisitizwa katika Qur'ani Tukufu.
Wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka nchi 40 duniani wanashiriki katika Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanachuo Waislamu ambayo yanafanyika katika vitengo vya kiraa na hifdhi. Mashindano hayo yataendelea hadi Januari 11.
727395