Hayo yamesemwa na Muhammad Husseini Yadegari Mkuu wa Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu nchini Iran katika sherehe za ufunguzi wa Mashindano ya Tatu ya Qur'ani ya Kimataifa ya Wanachuo Waislamu yanayoendelea katika mji mtakatifu wa Mash'had kaskazini-mashariki mwa Iran.
“Azma ya wanachuo na raghba yao ya kushiriki katika mashindano hayo ni katika kufuata mafundisho ya Qur'ani Tukufu”.
Amesema mashindano haya yatakuwa na athari kubwa kitaifa na kimataifa na kuzusha harakati kubwa ya Qur'ani nchini Iran hasa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Huku akisisitiza haja ya kubuni mazingira ya changamoto miongoni mwa wanachuo amesema kuwa, “ilhamu na changamoto ni nukta mbili zinazopatikana katika mashindano hayo jambo ambalo litainua kiwango cha mashindano na wanachuo”.
“Kuleta umoja miongoni mwa jamii za Waislamu, kuanzisha mitandao ya kijamii kwa msingi wa Qur'ani na kuwafanya wanafunzi wafahamu utamaduni wa kidini na Qur'ani wa nchi zingine na kutumia uwezo wa wanafunzi wa vyuo vikuu katika kufanikisha harakati ya Qur'ani ni kati ya malengo makubwa ya mashindano haya”, amesema Yadegari.
Akiashiria hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wanazuoni na wataalamu wa Qur'ani nchini Iran, amemnukulu Kiongozi Muadhamu aliposema kuwa, “Qiraa ya Qur'ani ni amali njema yenye thawabu na kwamba anayesoma zaidi Qur'ani kiu yake kwa kitabu hicho huwa kubwa zaidi”.
727397