IQNA

Taarifa ya Mashia wa Tunisia kuhusiana na matukio ya nchi hiyo

13:37 - January 19, 2011
Habari ID: 2067286
Jumuiya Utamaduni ya Ahlul Beit (as) ya Tunisia ambayo inafungamana na jamii ya Mashia wa nchi hiyo imetoa taarifa kufuatia matukio ya kisiasa ya hivi karibuni nchini humo ambayo yamepelekea kung'olewa madarakani utawala wa Dikteta Zainul Abidin bin Ali.
Taarifa hiyo imewasifu wananchi Waislamu wa nchi hiyo kutokana na juhudi zao kubwa za kuung'oa madarakani utawala huo mbovu uliokuwa ukipinga mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Jumuiya hiyo imesema kuwa raia wote wa Tunisia wana haki ya kufuatilia malengo na haki zao kwa njia za kisheria na amani jambo ambalo limebainishwa wazi katika katiba ya nchi hiyo na vilevile katika maazimio ya kimataifa.
Taarifa ya jumuiya hiyo imelaani vikali ufyatuaji ovyo wa risasi na kuuawa kiholela raia waliokuwa wakiandamana kwa amani wakifuatilia haki zao. Pia imelaani uporaji wa mali ya umma na kutaka wahusika wa jinai hizo dhidi ya taifa la Tunisia wafikishwe mbele ya vyombo uadilifu vya kisheria ili washughulikiwe vilivyo.
Vilevile imetaka viongozi wa serikali iliyong'olewa madarakani na wale wote waliohusika na ubadhirifu wa mali ya umma pamoja na utumiaji mbaya wa madarakana na ofisi wachunguzwe na kufikishwa mahakamani ili wajibu mashtaka yanayowakabili.
Mwishoni mwa taarifa hiyo Jumuiya ya Utamaduni ya Ahlul Beit (as) ya Tunisia imepinga vikali kila aina ya uingiliaji wa nchi za kigeni katika mambo ya ndani nchi hiyo na kuwataka Watunisia wote waimarishe na kuzingatia umoja na mshikamano wao wa kitaifa. 732732
captcha