Huku hisia dhidi ya Marekani zikiongezeka nchini Afghanistan, kanda za video za kushangaza na kushtua zimetolewa zikiwaonyesha wanajeshi wa Marekani wakiivunjia heshima Qur'ani Tukufu baada ya kuwaua raia Waislamu wasiokuwa na hatia katika kijiji kimoja cha Afghanistan.
Ripoti zinasema kuwa, kwa uchache raia watatu waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa katika hujuma ya wanajeshi vamizi wa Marekani dhidi ya madrasa ya Kiislamu ya mkoa wa Ghazni. Mwandishi wa kanali ya Press TV amesema wanajeshi wa Marekani waliifyatulia risasi Qur'ani Tukufu huku wakitusi matukufu ya Kiislamu.
Rais Hamid Karzai wa Afghansitan ameahidi kuchunguza kitendo hicho cha vikosi vya Marekani.
Wakati huo huo mamia ya Waafghani wenye hasira wameandamana katika mitaa ya mji wa Ghazni na kulaani hatua ya vikosi vya askari vamizi wa Marekani kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu na kuwaua raia kiholela katika eneo hilo.
Waafghani wanasema vikosi vya askari wa kigeni vinavyoongozwa na Marekani vinapuuza na kudharau utamaduni wa watu wa Afghanistan huku vikiwalenga raia wasio na hatia nchini humo. 736375