IQNA

Shakhsia wa Kishia waomboleza kifo cha Ayatullah Sheikh Muhammad Ali al-Amri

14:10 - January 26, 2011
Habari ID: 2070496
Wanazuoni wengi mashuhuri wa Kishia nchini Saudi Arabia na nchi nyinginezo za dunia wametoa taarifa mbalimbali wakituma salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha Ayatullah Sheikh Muhammad Ali al-Amri, kiongozi wa Mashia wa Saudia huko katika mji mtakatifu wa Madina.
Kiongozi huyo mashuhuri wa Waislamu wa Kishia wa Saudi Arabia aliaga dunia siku ya Alkhamisi tarehe 24 Januari baada ya kutoa huduma kubwa kwa madhehebu ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) kwa miaka mingi. Alikuwa na umri wa miaka 90. Akizungumzia suala hilo, Hassan Saffar Imam wa Swala ya Ijumaa ya mji wa Qatif Saudia ametoa taarifa akisema kuwa kifo cha alim huyo mkubwa ni mkasa, hasara, machungu na pigo kubwa kwa ulimwengu wa Kishia na Kiislamu kwa ujumla. Amesema, mwanazuoni huyo alikuwa mfano wa baba mwenye huruma na kiongoizi mwenye hekima kwa waumini wa mji mtakatifu wa Madina na marejeo ya wafanyaziara wa Kishia katika mji huo.
Sheikh Hassan Saffar amesema kuwa katika kipindi cha maisha yake, Sheikh al-Amri alipata na kuvumilia machungu mengi na kwamba alikuwa daima akimwomba Mwenyezi Mungu ampunguzie machungu yaliyompata kutokana na maradhi na uzee na wala hakuwa akilalamikia jambo lolote kuhusu hali yake hiyo.
Amesema kwamba alitumia muda wake mwingi kuwafundisha Waislamu darsa na mafunzo ya Akhlaki na maadili bora.
Sheikh Abdalla al-Yusuf, mwanazuoni mwingine mashuhuri wa Kishia wa Saudia ametoa taarifa akisema kuwa marehemu Ayatullah al-Amri alikuwa nembo ya elimu, subira, takwa, hekima, uzingatiaji dini na mapambano kwa ajili ya kutetea haki za Ahlul Bait wa Mtume (saw) na mtumishi mkuu wa waumini na wafanyaziara katika mji wa Madina.
Wanazuoni wengine wengi wa Kishia wakiwemo wa Iraq na Iran wametoa taarifa tofauti wakiomboleza kifo cha mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kishia nchini Saudi Arabia wakisema kuwa aliutoa umri wake wote kwa ajili ya mapambano na kuwahudumia Ahlul Bait wa Mtume (saw). 736376
captcha