Harakati za kimapinduzi zinazoshuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika hivi sasa ambayo yameanzia nchini Tunisia zimeenea hadi katika nchi nyingine na jambo hili linathibitisha uhakika kwamba wananchi wa eneo hili wameamka kwa kupata ilhamu kutoka kwenye mafundisho ya kidini na mwamko wa Kiislamu. Wananchi hao hivi sasa wanaonekana wamechoshwa na tawala za kibeberu na sasa wanataka wapate ukombozi wa kweli.
Wananchi wa Misri nao wanaonekana kutumia vizuri uzoefu wa kipekee wa zama hizi katika Mashariki ya Kati na sasa wameamua kujiamulia wenyewe mustakbali wao ikiwa ni pamoja na kupigania nafasi wanayostahiki kuwa nayo kieneo na kimataifa. Wananchi wa Misri na Tunisia wamechukua hatua ambayo wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa walikuwa hata hawadhani kabisa kwamba wangeliweza kuchukua. Maandamano ya mamilioni ya wananchi wa Misri yanaendelea hivi sasa kwa nia ya kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Rais Hosni Mubarak.
Itakumbukwa kuwa katika muongo wa 1960, Misri ilikuwa na nafasi muhimu sana katika ulimwengu wa Kiarabu lakini viongozi wa Cairo walilipotezea taifa hilo nafasi yake hiyo baada ya kuwa vibaraka wakuu wa Marekani kiasi kwamba leo hii, viongozi hao ndio wanaopata misaada mikubwa zaidi ya Marekani baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kama ilivyo katika nchi nyingine nyingi za Kiarabu, wananchi wa Misri na Tunisia wanakabiliwa na hali mbaya ya umaskini, ukosefu wa kazi sambamba na kukosekana demokrasia na utawala wa wananchi. Takwimu zinaonyesha kuwa karibu nusu ya wananchi wa Misri wana kipato cha chini ya dola mbili kwa siku hasahasa vijana wenye umri wa chini ya miaka 30.
Katika upande wa kisiasa pia, wananchi wa Misri hawana uhuru, na hilo lilithibitika kwenye uchaguzi wa mwaka jana ambao ulikumbwa na udanganyifu mkubwa sana. Ni jambo hilo ndilo linalowafanya wachambuzi wa mambo waamini kwamba, uendeshaji mbovu wa uchaguzi huo umechangia pakubwa katika kukasirika wananchi na kuamua kujitokeza kwa mamilioni katika maandamano yanayoendelea hivi sasa, yanalenga kuipindua serikali ya kidikteta ya Husni Mubarak. Jambo lisilokanushika hivi sasa ni kwamba eneo nyeti la Mashariki ya Kati linashuhudia mabadiliko ya aina yake, naam, mapinduzi makubwa ya wananchi. Mabadiliko hayo yanakwenda kwa kasi kubwa sana kiasi kwamba tawala zisizo za kidemokrasia katika eneo zinaonyesha wazi hofu yao na hata hatua za tawala hizo za kuwakandamiza zaidi wapinzani zimeshindwa kuzisaidia chochote tawala hizo.
Kuna baadhi ya wachambuzi wa mambo wanajaribu kupotosha mapinduzi yanayoshuhudiwa katika eneo hivi sasa kwa kuyaita ni mapinduzi ya watu wenye njaa. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa mapinduzi hayo yametokana na kurejea wananchi wa nchi hizo katika asili yao ya kupenda mafundisho ya dini yao tukufu ya Kiislamu. Wananchi wamechoshwa na tawala zisizoheshimu dhati za kidini za wananchi hao.
Rais Hosni Mubarak wa Misri ametoa ahadi za kufanya mabadiliko makubwa ndani ya uongozi wake lakini wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kama ambavyo mbinu hiyo haikusaidia huko Tunisia, wananchi wa Misri nao hawatakubali kuhadaiwa bali wanaonekana wataendelea na maandamano yao hadi watakapoupindua utawala wa kidikteta wa Hosni Mubarak.
741368