IQNA

Rais Ahmadinejad asema dunia inahitaji mfumo mpya wa usimamizi

14:31 - February 20, 2011
Habari ID: 2083704
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa baada ya kusambaratika kimaxi na mfumo wa ubepari, ulimwengu sasa unahitajia mfumo mpya wa nadharia na usimamizi.
Rais Ahmadinejad ameyasema hayo Jumamosi usiku alipokutana na wageni wanaoshiriki katika Kongamano la 24 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran. Rais Ahmadinejad ameongeza kuwa madola ya kibeberu yenye kiburi ndio kizingiti kikubwa zaidi katika njia ya mwanadamu katika kufikia ukamilifu na kuanzishwa utawala wa dunia kwa msingi wa tauhidi na uadilifu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Wamaxi na viongozi wa mfumo wa kibepari walikalia kwa mabavu ardhi za Palestina kwa malengo ya kikoloni kupitia hadaa. Amesema wakoloni hao waliwakusanya watu kutoka maeneo mbalimbali duniani na kuwapelekea katika ardhi za Palestina huku wakaazi asili wa eneo hilo wakilazimishwa kuwa wakimbizi. Rais Ahmadinejad ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 65, mabeberu wamelazimisha vita mara tano katika eneo la Mashariki ya kati kwa visingizio mbalimbali jambo ambalo limekuwa kizingiti katika harakati za maendeleo za eneo hli.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema dunia inakaribia kushuhudia matukio makubwa. Amesema uwezo mkubwa wa mataifa ambao bado haujatumika utatumika katika kumletea mwanadamu heshima na uadilifu. Amesema kuwa nguzo za madola ya kibeberu yenye kiburi zinaanguka moja baada ya nyingine. Ametoa bishara njema kuwa, kwa rehma ya Mwenyezi Mungu, katika mustakabali wa karibuni kutakuwepo dunia isiyo na Wazayuni, madola ya kibeberu na mataghuti.
Kongamano la 24 la Kimataifa la Umoja baina ya Waislamu lilianza jana mjini Tehran kwa hotuba ya Spika wa Bunge la Iran Dkt. Ali Larijani. Wasomi na wanafikra 250 kutoka nchi 57 duniani wanashiriki katika kongamano hilo ambalo hufanyika kila mwaka kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu.
750807
captcha