Akizungumza katika Mkutano wa 24 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu uliofanyika hivi karibuni mjini Tehran, Mufti Ceric ameongeza kuwa msimu wa ibada ya hija ni wakati wa kuonyesha umoja wa mshikamano wa Waislamu wote. Amesema kuna haja ya Waislamu kudumisha umoja na kutegemea thamani za Kiislamu. Mufti huyo ameongeza kuwa hitilafu miongoni mwa Waislamu hazina mizizi katika dini bali zinatokana na sababu za kisiasa.
"Umoja unaweza kupatikanaje? Kwa maoni yangu Waislamu duniani ni kitu kimoja na hawana hitilafu. Mifarakano iko miongoni mwa maulamaa na wanasiasa", amesema.
Dr.Ceric ametoa wito kwa maulamaa na wasomi wa Kiislamu kuwa waangalifu ili wasitumbukie katika mitego ya maadui na amewataka wazungumze kwa sauti moja kwa mujibu wa mafundisho na thamani za Kiislamu.
Mwanazuoni hiyo wa Bosnia ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zake za kuunga mkono Uislamu na Waislamu.
Mkutano wa 24 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulifanyika Februari 19-21 mjini Tehran na uliandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha Madhehebu ya Kiislamu. 750634