Kwa mujibu wa tovuti ya Palestineinfo, Hassan Khater Katibu Mkuu wa kamisheni hiyo ametoa taarifa akitangaza kuwa kikao hicho kimepangwa kufanyika tarehe 29 hadi 31 za mwezi huu wa Machi ambapo utawala ghasibu wa Israel umewaalika mawaziri wa utalii kutoka nchi 30 za dunia kuhudhuria kikao hicho.
Khater amesema kuwa udhibiti wa utawala huo huko Quds ni kinyume na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limezitaka nchi wanachama wake kutotambua rasmi madai ya utawala huo wa Tel Aviv kuhusu mji huo mtakatifu wa Waislamu na Wakristo. Amesema kufanyika kwa kikao hicho ni ishara ya wazi kwamba utawala huo unataka kusisitiza kimataifa kwamba mji huo ni mji mkuu wake.
Hassan Khater amezitaka nchi zilizoalikwa kuhudhuria kikao hicho kutojibu mwaliko huo na badala yake zilaani hatua hiyo ya utawala haramu wa Israel.
Utawala wa Israel uliteka na kukalia kwa mabavu sehemu ya mashariki ya Quds katika vita vyake na Waarabu mwaka 1967, na tokea wakati huo hadi sasa umekuwa ukijenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika mji huo licha ya kuwepo upinzani mkali wa kimataifa kuhusu suala hilo. 756199