Harakati hiyo imetambuliwa rasmi na kupewa kibali cha kuendesha shughuli zake na Wizara ya Mambo ya Ndani mara tu baada ya kujiuzulu Muhammad Ghanushi, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Tunisia na kuchukuliwa nafasi yake na al-Baji Faid as-Sibsi.
Harakati ya an-Nahdha iliasisiwa nchini Tunisia mwaka 1981 na Rashid Ghanushi pamoja na wasomi kadhaa wa Tunisia waliokuwa wameathirika na harakati ya Ikhwanul Muslimeen nchini Misri.
Harakati hiyo ilipigwa marufuku mwaka 1989 na serikali dhalimu ya dikteta Zeinul Abedeen bin Ali aliyeng'olewa madarakani hivi karibuni na wimbi la maandamano ya wananchi, baada ya kushiriki kwenye uchaguzi wa bunge na kujishindia asilimia 17 ya kura zilizopigwa. Baada ya hapo wanachama wake wengi walikandamizwa, kuteswa na kufungwa jela.
Rashid Ghanushi aliruhusiwa kurejea nchini Tunisia hivi karibuni baada ya kulazimika kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 20. 756479