Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, takribani Waislamu 50,000 kutoka Kenya na nchi kadhaa duniani walishiriki katika sherehe za Milad un Nabii mwaka huu mjini Lamu. Mjumuiko huu mkubwa zaidi wa Waislamu katika eneo la Afrika Mashariki na Kati uliwaleta pamoja Waislamu katika Msikiti wa Riyadha kwa lengo la kusoma Maulidi.
Kilele cha sherehe hizo za Maulidi zilizoanza Jumatatu 24 Mfunguo Sita-Rabi ul Awwal ( Februari 28) kilikuwa Ijumaa 28 Mfunguo Sita-Rabi ul Awwal (4 Machi 4) ambapo maelfu ya Waislamu walizuru kaburi la mwanzilishi wa Maulidi ya Lamu Habib Swaleh Jamal Leyl ambaye alianzisha Maulidi mwaka 1866. Aidha katika siku hiyo kulikuwa na Zefe katika barabara kuu ya Lamu ambapo washiriki walisoma Qasida za kumsifu Mtume SAW.
Kati ya walishiriki ni rais mstaafu wa Tanzania Ustadh Ali Hassan Mwinyi, Mufti wa Comoro Sheriff Twahir Maulana na Mshauri wa Wizara ya Mafuta ya Omna Khalifa Bin Mubarak Al Hinani. Aidha Mkuu wa Idara ya Utamaduni ya Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Nairobi Bw. Abbas Farmand vile vile alishiriki katika sherehe hizo za Maulid.
Mratibu wa Maulid ya Lamu Sheikh Muhdhar Khitamu amesema karibu Shilingi Milioni 12 za Kenya zilitumika kugharamia sherehe za Maulid mwaka huu.
Katika sherehe hizo za Maulid kulikuwa pia na kambi ya matibabu ya bure katika eneo la Msikiti wa Riadha na vilevile wafanyakazi wa afya 100 waliojitolea kutoka Kenya, Uhispania na Uingereza walitoa huduma kwa walioshiriki katika Maulid.
Maimamu kutoka kote nchini Kenya pia walishiriki katika kongamano kuhusu usimamizi wa Kiislamu katika majimbo yao. Aidha waliadili mbinu za kupambana na ugaidi. Mbali na Sherehe za Milad un Nabii zilizojumuisha mihadhara ya kidini, mashindano ya Qur'ani na ibada za usiku, vilevile kulikuwa na tamasha za kiutamaduni.
758804