Mohammad Reza Dehshiri alikuwa akizungumza Machi 8 mjini Tehran katika sherehe kuzinduliwa tarjuma mpya ya Qurani kwa lugha ya Kihispania.
Amesisitiza kuwa kuna haja ya kuzingatiwa zaidi suala la kutarjumi Qurani kwa lugha zote duniani ili kuwafahamisha walimwengu kuhusu mafundisho halisi ya Uislamu na Qurani na kwa njia hiyo kukabiliana na propaganda potofu dhidi ya dini tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Akisisitiza kuwa mitazamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejengeka katika msingi wa Qurani, Dehshiri amesema ICRO inatilia mkazo suala la kueneza utamaduni wa Kiislamu kwa mujibu wa nasaha za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Hujjatul Islam Asghar Saberi Mkuu wa Taasisi ya Kuratibu Tarjuma na Uenezaji Mafundisho ya Kiislamu amesema kuna haja ya kutarjumi Qurani Tukufu kwa lugha mbali mbali. Amekumbusha kuwa Bibilia tayari imeshatarjumiwa kwa lugha zaidi ya 2500 ilihali Qurani Tukufu imetarjumiwa kwa lugha 150 tu.
Tarjuma mpya ya Qurani kwa lugha ya Kihispania imetayarishwa na Jaafari Gonzales. Gonzales alizaliwa katika familia ya Kimaxi mwaka 1950 katika mji mkuu wa Uhispania Madrid. Baada ya miaka kadhaa ya kutafakari na kutafuta ukweli, alisilimu mwaka 1983. Baada ya mwaka moja alioana na mwanamke Mhispania ambaye pia alikuwa amesilimu.
Nuskha 15000 zilichapishwa katika chapa ya kwanza ya tarjuma hiyo na kuna mipango ya kuchapisha nuskha zingine laki moja ambazo zitasambazwa katika nchi kama vile Bolivia, Venezuela, Argentina, Cuba, na Colombia.
760477