Hayo yamesemwa na Naibu Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) Sayyid Shahabuddin Sadr katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa kuhusu 'Nafasi ya Imam Musa Sadr katika Mwamko wa Kiislamu Duniani' lililofanyika Machi 12 mjini Tehran.
Ameashiria aya ya Qur'ani Tukufu inayosema: "Miongoni mwa waumini wapo watu waliotimiza waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwishakufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo", na kusema Imam Musa Sadr alikuwa Muislamu halisi na alikuwa dhihirisho la aya hiyo.
Kupambana na umasikini na ufisadi kupitia mikakati maalumu ni kati ya mambo yaliyopewa umuhimu na Imam Musa Sadr.
Shahabuddin Sadr amesema Bunge la Iran linafuatilia hatima ya Imam Musa Sadr kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran. Ameelezea matumaini yake kuwa umma utapokea habari nzuri za kurejea Imam Musa Sadr nyumbani baada ya kutoweka miaka 32 iliyopita.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, Imam Mussa Sadr, raia wa Lebanon mzaliwa Iran, alitoweka mwaka 1978 akiwa nchini Libya, baada ya kufanya safari ya mzunguko katika nchi kadhaa za Kiarabu na hatimaye kuelekea nchini Libya kwa mwaliko wa Gaddafi, lakini kabla ya kuondoka nchini humo alitekwa nyara pamoja na wasaidizi wake, na hadi leo hawajulikani walipo. Serikali ya Libya inadai kwamba Imam Mussa Sadr aliondoka nchini humo na kuelekea Italia, wakati ambapo vyombo vya upelelezi vya Italia na Lebanon vinathibitisha kwamba shakhsia huyo wa kidini hakuwahi kuondoka katika ya ardhi ya Libya.
762520