Muungano wa Maulama wa Kiislamu umetahadharisha dhidi ya mauaji yanayofanywa na serikali ya Yemen dhidi ya waandamanaji wa nchi hiyo wanaopigania haki zao, na wakati huohuo kutangaza uungaji mkono wake kwa waandamanaji hao.
Muungano huo unaoongozwa na Sheikh Yusuf Qardhawi umezitahadharisha serikali za Kiarabu dhidi ya kukandamiza na kuwaua waandamanaji wanaoandamana kwa amani.
Huku ukitoa taarifa ya kuwaunga mkono watu wa Yemen, Muungano wa Maulama wa Kiislamu umesema kuwa utaendelea kuwaunga mkono waandamanaji wa Yemen maadamu wataendelea kupigania kwa amani haki zao ambazo zimeainishwa na kuwekwa wazi katika maazimio ya kimataifa ya haki za binadamu.
Muungano huo umelaani vikali ukandamizwaji unaofanywa na serikali ya Yemen dhidi ya waandamaji na kubainisha wazi wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na hali ya mambo nchini humo. Umewataka waandamanaji kuwa na subira na kuendelea kusisitiza juu ya kupewa haki zao kwa njia ya amani na isiyo ya umwagaji damu. 765097