IQNA

Iran yataka waliochoma moto Qur'ani tukufu huko Marekani washtakiwe

15:41 - March 26, 2011
Habari ID: 2098088
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameelezea wasi wasi kwa kuhusu kuendelea vitendo vya kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu huko Marekani na kuitaja hatua ya kuchomwa moto Qurani hivi karibuni kuwa yenye chuki. Aidha Iran imetaka waliotekeleza kitendo hicho cha kuivunjia Qurani heshima wafikishwe kizimbani.
Romin Mehmanparast ameitaka serikali ya Marekani kuchukua hatua za kuzuia chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.
Wakati huo huo Iran imeutaka Umoja wa Mataifa ulaani hatua ya kanisa moja la Florida nchini Marekani ya kuchoma moto Kitabu Kitakatifu cha Waislamu yaani Qur'ani. Aidha Tehran imetaka wahusika wa uhalifu huo kufikishwa mbele ya sheria. Mohammad Khazaei Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, kitendo hicho kimewakera na kuwakasirisha Waislamu wote duniani na kwamba vitendo kama hivyo vya kichokozi ni hatari na vinaweza kuzusha machafuko makubwa. Tarehe 20 Machi mhubiri mmoja wa kilokole nchini Marekani Wayne Sapp alichoma moto kopi ya Qur'ani tukufu katika kanisa moja dogo la Florida. Maulamaa wengi wa Kiislamu wamesema kuwa, hatua hiyo ya kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu inatokana na uadui na kampeni za kuwafanya Wamarekani wauchukie Uislamu. Kitendo hicho kimelaaniwa na Waislamu duniani huku baadhi yao wakiandamana katika maeneo mbalimbali.
764863

captcha