IQNA

Iran yaadhimisha 'Siku ya Jamhuri ya Kiislamu'

12:41 - March 31, 2011
Habari ID: 2099302
Katika kalenda ya minasaba ya Iran, siku ya tarehe 12 Farvardin Hijria Shamsia sawia na Aprili Mosi Miladia imepewa jina la Siku ya Jamhuri ya Kiislamu. Siku hii imetajwa kuwa siku ya ushindi wa haki dhidi ya batili.
Miaka 32 iliyopita katika siku kama hii katika hali ambayo ilikuwa haijapita miezi miwili tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuangushwa utawala wa kifalme, wananchi wa Iran walishiriki katika kura ya maoni au kura ya maamuzi ya kitaifa na hapo wakachagua Jamhuri ya Kiislamu kuwa mfumo wa kuiongoza kisiasa Iran. Katika kura hiyo ya maoni asilimia 98.2 ya watu walipiga kura ya kubadilisha mfumo wa kisiasa na kijamii nchini. Tukio hilo muhimu limetajwa kuwa nukta muhimu katika historia na hatima ya taifa la Iran.
Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran ni mfano mzuri wa wananchi kujiamulia mustakabali wao na jamhuri inaashiria kushiriki kikamilifu wananchi katika kuchagua na kujiamulia mfumo wautakao. Jambo hilo linabainika wazi katika kipindi cha miaka 32 iliyopita ambapo taifa la Iran limeshiriki katika uchaguzi kwa wastani mara moja kwa mwaka katika chaguzi mbali mbali.
Katika siku hii ya kihistoria, nafasi nyeti na muhimu ya wananchi kujiamulia mustakbali wao ilibainika wazi. Siku hii kwa hakika ni kutimizwa nara ya 'kujitawala, uhuru na Jamhuri ya Kiislamu'. Siku ya Jamhuri ya Kiislamu inaashiria namna taifa la Iran lilivyo na uhuru kamili na kwamba kamwe halitaruhusu madola ya kigeni kuingilia suala la kujiamulia hatima yake.
Kura ya taifa la Iran kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu tokea mwanzo ilikuwa na ujumbe wenye mfano wa kuigwa.
Imam Khomeini MA muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa kufanyika kura ya maoni ni moja kati ya misingi ya kuanisha mustakabali wa mfumo wa kisiasa wa Iran. Uono huu wa mbali wa Imam katika kipindi nyeti cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni jambo ambalo liliimarisha nguzo za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Busara ya Imam Khomeini iliwathibitishia wazi wanaodai kuwa watetezi wa uhuru na uadilifu, namna Mapinduzi ya Kiislamu yalivyopata ushindi kwa ajili ya kuleta uadilifu.
Kura hiyo ya maoni iliyopigwa kwa njia za demokrasia ilisisitiza nukta hii kuwa wananchi ndio wamiliki halisi wa mapinduzi wanayoyaunga mkono. Hii ndio sababu katika kura hiyo ya maoni kulikuwa na machaguo mawili ya 'ndio' au 'la' kwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Utawala wa wananchi una misingi miwili, kwanza ni kushiriki wananchi katika medani na natija ya kushiriki huku ni kubuniwa mfumo wa kisiasa na aina ya serikali. Msingi wa pili wa utawala wa wananchi katika mifumo ya demokrasia ni kuainisha vigezo vya mfumo wa kuitawala jamii ambao huainisha fremu ya idiolojia ya kisiasa ya jamii mbali na kuwa kielelezo cha thamani zinazofuatwa na mfumo unaotawala pamoja na mipaka ya kifikra na misingi ya kisiasa. Kwa hivyo kura ya 'ndio' ya taifa la Iran ya kutaka kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu si tu kuwa lilikuwa chaguo la kidemokrasia bali pia kura hiyo kwa kuingia katika uga wa idolojia ya thamani za kidini iliainisha mkondo wa harakati ya mfumo kwa msingi wa thamani za kidini na kibinaadamu.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliasisiwa kwa mujibu wa kura za wananchi katika kura ya maoni ya 30 na 31 Machi 1979 katika msimu wa kwanza wa machipuo baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu Februari 11 1979. Aina ya serikali nchini Iran ni Jamhuri ya Kiislamu na kuwepo mfumo wa Kiislamu ni kwa mujibu wa katiba na huo ni msingi ambao hauwezi kubadilika.
Hatua ya kuwataka wananchi wa Iran wapige kura ya kuainisha uungaji mkono wao kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo ambalo limeyafanya mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yawe ya kipekee na yasiyo na kifani duniani. Kura ya maoni ya tarehe 30-31 Machi 1979 ilifanyika kwa ujumbe wa Imam Khomeini MA. Wakati huo, Imam Khomeini alikumbusha nukta muhimu na akabainisha kuwa kura hiyo ya maoni ilikuwa ni kura kwa ajili ya uhuru na kujitawala. Aliongeza kuwa taifa la Iran lilikuwa na haki ya kupigia kura serikali liitakayo. Ujumbe huo wa Imam uliashiria ufahamu na imani kamili ya Imam kuhusu busara na uwezo wa kisiasa wa taifa la Iran. Katika kipindi hicho muhimu, baada ya ushindi wa Mapinduzi ambapo maadui walikuwa wakitafuta kila fursa ya kuyasambaratisha mapinduzi, wananchi wa Iran waliuchagua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa wingi mkubwa wa kura. Kwa natija hiyo zilisambaratika njama zote zilizokuwepo za kuibua mgawanyiko katika mkondo wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Leo baada ya kupita miongo mitatu tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, moja ya vipimo vya ustawi wa kisiasa wa Iran ni kutegemea kura ya wananchi na kuwepo mfumo wa utawala wa wananchi au demokrasia.
Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaingia katika muongo wa nne wa uhai wake uliojaa thamani ambapo sasa ni mfano wa kuigwa kuhusu namna ya kufungamana na maadili na umaawi katika siasa. Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa ni mfano wa kuigwa na mataifa yote yanayotaka uhuru kamili na uadilifu duniani. Uzoefu wa mapinduzi makubwa kote duniani unaonyesha kuwa kubuniwa mfumo wa kisiasa ingawa kidhahiri hufanyika kwa msingi wa ushirikishi wa kisiasa, kura na uchaguzi, lakini harakati hii hudhoofika na kupotea kutoka mkondo wake na hatimaye kusahaulika thamani na misingi ya awali. Hii ni katika hali ambayo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeweza kudumu na kuwa endelevu kutokana na kufungamana na kusimama kwa mujibu wa thamani za Mwenyezi Mungu na demokrasia ya kidini katika fremu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Katika uga wa kitaifa na kimataifa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unafuata mkondo wa ustawi na utandawazi.
Katika kipindi cha miaka 32 iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu imekabiliana na njama kama vile vita vya kulazimishwa na vikwazo vingi. Katika kukabiliana na njama hizi Iran imesimama kidete bila kutikisika na hili linatokana na kuwa waangalifu wananchi na viongozi wa mfumo wa Kiislamu.
Pamoja na hayo, maadui wamekuwa wakijaribu kuonyesha kuwa thamani za Kiislamu na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu ni jambo ambalo haliwezi kuenda sambamba na ustawi wa nchi. Lakini kinyume na madai hayo, Iran imepiga hatua kubwa za maendeleo kutokana na kusimama imara mbele ya mashinikizo ya maadui. Baadhi ya maendeleo makubwa ya Iran yanaonekana katika sekta za teknolojia ya nyuklia. Iran sasa ni kati ya nchi chache sana duniani zinazomiliki teknolojia muhimu ya nyuklia. Hii ni katika hali ambayo madola makubwa ya kibeberu na istikbari yalikuwa na dhana potofu kuwa yangeilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulegeza misimamo na kuzuia maendeleo yake kupitia vikwazo, mashinikizo ya kisiasa, vita vya kulazimishwa na kuibua mifarakano nchini. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kusambaratisha njama hizo za maadui na kufuatia mkondo wa ustawi ambao imejiainishia yenyewe.
Iran inaadhimisha Siku ya Jamhuri ya Kiislamu katika hali ambayo imepitia kipindi kigumu huko nyuma na sasa inalenga kufikia katika kilele cha ustawi wa kielimu na kisayansi. Aidha katika uga wa siasa za kieneo na kimataifa Iran imeweza kutoa changamoto kubwa kwa madola ya kibeberu yanayodai kutetea uhuru na demokrasia. Hivi sasa kwa ustawi wa kielimu na kisiasa Iran imefanikiwa kuwa kigezo cha utawala kwa mujibu wa misingi ya kidini, kimaanawi na kutetea uadilifu. Iran sasa ni kituo cha matukio na ubunifu wa kisiasa Mashariki ya Kati na dunia nzima.
Azma ya taifa la Iran ya kutaka kusimama kidete, kujitegemea na kulinda izza yake ni misingi muhimu na vigezo vya kitaifa katika kufikia malengo ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Johari halisi ya misingi hiyo ni kupinga satwa ya kibeberu na kusimama kidete mbele ya madola ya kibeberu yanayotumia mabavu. Kwa msingi huu ushindi na mafanikio ya Iran katika miongo mitatu iliyopita ni kigezo, ilhamu na chanzo cha matumaini kwa mataifa ambayo yanafuatilia malengo ya mapinduzi ya Kiislamu na yanayofahamu thamani halisi za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Suala hili ni chanzo cha kuzidi kina cha mkondo wa mwamko baina ya mataifa ya dunia hasa yaliyodhulumiwa duniani. Hivi sasa pamoja na kuwepo njama na propaganda za Wamagharibi dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuenezwa chuki dhidi ya Uislamu, athari za Mapinduzi ya Kiislamu katika mataifa mbali mbali duniani ni ukweli usioweza kupingika. Pamoja na kuwa njama za maadui dhidi ya taifa la Iran zinaendelea kwa visingizio mbali mbali, lakini kama uzoefu ulivyoonyesha huko nyuma Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea na mkondo wake wa kufika kilele cha ustawi wa kielimu, kisisiasa na kidini.
767207

captcha