IQNA

Tunisia yaruhusu Hijab katika vitambulisho

13:29 - April 03, 2011
Habari ID: 2099807
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imesema itawaruhusu wanawake wa nchi hiyo kuvaa Hijabu ya Kiislamu wakati wakipiga picha za kitambulisho.
Hatua hiyo ni kufuatia mapinduzi ya Watunisia yaliyopelekea kutimuliwa dikteta wa nchi hiyo Zine el Abidine Ben Ali mapema mwaka huu.
Hijabu ilipigwa marufuku Tunisia mwaka 1993.
“Hatua hii inaenda sambamba na marekebisho yanayolenga kustawisha misingi na thamani za mapinduzi ya Tunisia ya mwezi Januari na vile vile kulinda haki za umma na kiraia”, imesema taarifa ya wizara hiyo.
Utawala wa kiimla wa Ben Ali ulikuwa umepiga marufuku vazi za Hijab katika taasisi zote za kiserikali na vyuo vikuu. Wanawake wa Tunisia walikuwa wanalazimishwa na utawala uliotimuliwa wa Ben Ali kutia saini ahadi ya kutovaa hijabu katika idara za serikali.
Hivi karibuni vile vile Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia iliwaruhusu wanaume kupiga picha za vitambulisho pasina kukata ndevu. Punde baada ya mapinduzi ya Tunisia adhana pia ilianza kusikika katika Misikiti ya nchi hiyo na sala za jamaa na Ijumaa zilianza kusaliwa baada ya kupiga marufuku kwa muda mrefu.
767812
captcha