IQNA

Utawala wa Ufaransa washadidisha hatua za chuki dhidi ya Uislamu

10:09 - April 08, 2011
Habari ID: 2102131
Hatua ya chama tawala nchini Ufaransa cha UMP ya kuanzisha mjadala juu ya Uislamu imekabiliwa na radiamali kubwa za ukosoaji za Jumuiya za Kiislamu, vyama vya mrengo wa kushoto na hata vya mrengo wa kulia vya nchi hiyo.
Jumuiya za Kiislamu za Ufaransa zimeeleza kuwa kuanzisha mijadala ya aina hiyo kutaamsha na kuchochea hisia za watu. Mjadala huo unalenga kuonyesha kuwa kuna mgongano kati ya mfumo wa Kisekula wa Ufaransa na utekelezaji wa hukumu na mafundisho ya Kiislamu, ili kwa njia hiyo kuandaa mazingira ya kuwawekea mipaka na kuwabana zaidi Waislamu wa nchi hiyo. Kabla ya kufanyika kongamano hilo la mjadala juu ya Usekula na Uislamu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Claude Gueant alitoa matamshi ya kuonyesha chuki za serikali ya Paris kwa madhihirisho ya Uislamu kwa kueleza kwamba masuala kama vile vyakula halali, kutekeleza ibada za Sala mabarabarani na kutotumia Waislamu mabwawa ya kuogelea yenye mchanganyiko wa wanawake na wanaume yamesababisha matatizo mengi kwa nchi hiyo. Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa yametolewa katika hali ambayo mnamo mwezi uliopita Rais wa nchi hiyo Nicolas Sarkozy alisema katika hotuba aliyotoa kupitia redio na televisheni kama ninavyomnukuu: "Hatutaki kuwa na jamii ambayo ndani yake kuna tamaduni ndogondogo zinazojitangazia uwepo wao bila kuchanganyika na tamaduni nyinginezo." Sarkozy akaendelea kueleza kwamba: "Nchi ya Ufaransa haikaribishi watu ambao hawawezi kuchanganyika kwenye utamaduni wa watu wa nchi hii na kujioanisha na utamaduni huo." Mwisho wa kumnukuu. Kabla ya Rais wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri Mkuu wa zamani wa Australia John Howard na Waziri Mkuu wa zamani wa Uhispania José María Aznar walishatamka bayana kuwa wanapinga kustawi tamaduni nyingine huko Magharibi. Ufaransa, inayojinasibu kuwa ni kitovu cha demokrasia ndiyo iliyoko mstari wa mbele katika kushadidisha chuki na kueneza khofu dhidi ya Uislamu katika ulimwengu wa Magharibi. Ikumbukwe kuwa kuwapiga marufuku wanafunzi wa kike wa Kiislamu wasivae hijabu mashuleni kulianzia Ufaransa na kuenea katika nchi nyingine za Magharibi.
Hatua za Sarkozy na serikali yake ya chama cha UMP za kuanzisha kampeni za chuki dhidi ya Uislamu hazitokani na mitazamo tu ya kiongozi hiyo iliyo dhidi ya Waislamu; bali kuna sababu nyingine iliyomsukuma Rais huyo wa Ufaransa kuchukua hatua hizo. Hivi sasa Sarkozy anakabiliwa na hali ngumu kisiasa, kwani ni miezi 14 tu imesalia kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo. Wakosoaji wa Sarkozy, vikiwemo vyama vya mrengo wa kushoto na washindani wake wa mrengo wa kulia wanaelezea sababu ya Rais wa Ufaransa kutekeleza sera na hatua za chuki dhidi ya Uislamu kwa kueleza kwamba Sarkozy anafanya hivyo ili kwanza kuzibabaisha fikra za walio wengi zisishughulishwe na utendaji wake mbovu wa kushindwa kuboresha hali ya uchumi wa nchi hiyo. Lakini pili, anafanya hayo ili kuvutia kura za wafuasi wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu mpaka. Kwani uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa Sakrozy ameachwa nyuma na Marine Le Pen, kiongozi wa Mrengo wa Kitaifa ambao ni chama cha mrengo wa kulia chenye misimamo ya kufurutu mpaka na chuki pia dhidi ya Uislamu.
768640
captcha