IQNA

Dharau dhidi ya Qur'ani Tukufu haikubaliki na inatokana na mughafala

12:13 - April 16, 2011
Habari ID: 2106286
Akijibu barua ya Mwakilishi wa Kudumu wa Jamuri ya Kiislamu katika Umoja wa Mataifa kuhusiana na hatua ya dharau ya kuchomwa moto Qur'ani Tukufu katika jimbo la Florida huko Marekani, Ban Ki Moon Katibu Mkuu wa umoja huo kwa mara nyingine tena amekemea na kulaani kitendo hicho na kusisitiza kwamba kukosewa heshima kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu ni jamo la kusikitisha, lisilokubalika na linalotokana na mughafala.
Kwa mujibu wa tovuti ya Masrawy, Ban Ki Moon amesema kuwa kukosewa heshima Qur'ani ni jambo linalopingwa vikali na kuongeza kuwa kuna watu waovu na wasiojali nyuma ya kitendo hicho, ambao wanataka kuchochea vitendo vya kutovumiliana kati ya watu wa jamii mbalimbali na kwamba umoja huo utaendelea kushajiisha mielekeo na fikra za kuleta amani na maelewano miongoni mwa wafuasi wa dini tofauti. Huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo maelewano kati ya watu wa jamii na utamaduni tofauti duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa mielekeo ya kufurutu ada na mipaka haina nafasi tena katika mwenendo wa mazungumzo kati ya staarabu mbalimbali. Amesema watu wanaoeneza na kuchochea hisia za chuki za kidini hawapasi kupewa fursa ya kueneza mitazamo yao hiyo hatari kwenye jamii.
Hivi karibuni Muhammad Khazai, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa alimwandikia barua Katibu Mkuu wa umoja huo akimtaka achukue msimamo thabiti na wa wazi katika kulaani kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu na kasisi muovu Terry Jones wa jimbo la Florida na hivyo kuamsha hasira ya Waislamu katika pembe mbalimbali za dunia. 774680
captcha