Mwamko wa wananchi unaokwenda sambamba na umwagaji damu Bahrain ulianza Februari 14 mwaka huu na ungali unaendelea huku utawala wa kifalme nchini humo ukijaribu kuukandamiza bila mafanikio. Utawala wa kifalme wa Aal Khalifa unapata uungaji mkono mkubwa wa Saudi Arabia na Marekani katika kukandamiza mwamko wa Kiislamu wa wananchi. Utawala huo sasa umeenda mbali zaidi na kuanza kubomoa na kuteketeza kwa moto misikiti. Hadi sasa misikiti karibu 30 ya Bahrain imebomolewa au kuteketezwa kwa moto. Misahafu iliyokuwa ndani ya misikiti hiyo pia imeteketezwa kwa moto na vikosi hivyo vya Bahrain vikisaidiwa na wanajeshi vamizi wa Saudi Arabia. Ili kulalamikia jinai hiyo ya kuchomwa moto Qurani Tukufu na kuvunjwa misikiti wananchi waumini wa Bahrain leo Ijumaa waliitangaza kuwa ‘Ijumaa ya Qurani Tukufu.' Jumuiya ya al Wefaq ya Bahrain ndiyo iliyoitisha maandmano ya leo. Chama hicho kimeuonya utawala wa Aal Khalifa kuhusu hatua zake za kuwakandamiza wananchi wasio na hatia wa Bahrain.
Ripoti zinasema vikosi vya Bahrain vikiwa vinapata himaya ya wanajeshi wa Saudia vimewafyatulia risasi waandamanaji waliojitokeza baada ya sala ya Ijumaa kulaani kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu na kuchomwa moto Kitabu hicho kitakatifu cha Mwenyezi Mungu. Vifaru vimemiminika barabarani katika miji kadhaa ya Bahrain kukabiliana na wananchi wenye hasira.
Ali Salman Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya al Wefaq nchini Bahrain ameashiria kuongozeka machafuko nchini humo na kusema watawala wa familia ya kifalme ya Aal Khalifa katika ukandamizaji wao wa maandamano ya wananchi wanafanya maangamizi ya kimbari.
Maandamano ya Bahrain ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miezi mitatu sasa yameingia katika ukurasa mpya. Mbali na kuongezeka idadi ya watu wanaouawa na kujeruhiwa, kufutwa kazi wafuasi wa upinzani wakiwemo madaktari, walimu na hata wanamichezo sasa utawala wa Aal Khalifa umesonga mbele zaidi na kubomoa misikiti na vituo vya Kiislamu.
Hussein Abdullah mtetezi wa haki za binaadamu Bahrain ameiambia kanali ya al Alam kuwa, maamuzi kuhusu siasa za Bahrain sasa yanachukuliwa katika mji mkuu wa Saudi Arabia Riyadh. Hussein Abdullah amelaani vikali hatua ya vikosi vya Bahrain na wanajeshi vamizi wa Saudia ya kuivunjia heshima Qurani Tukufu na misikiti. Waandamanaji nchini Bahrain wamesema hawatalegeza misimamo yao ya kutaka kuuondoa madarakani utawala wa Aal Khalifa ambao pia unapata uungaji mkono wa Marekani. Aidha vyama vya upinzani vimeanzisha kampeni ya kimataifa chini ya anuani ya ‘Misikiti Yetu, Maisha Yetu' ili kulaani sera za kuvunjwa misikiti na utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain. Maandamano makubwa yamefanyika pia nchini Iran na katika nchi kadhaa duniani kulani hatua ya wanajeshi wa Bahrain na Saudia ya kuchoma moto Qurani Tukufu.
778648