Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na shirika la PEW, wananchi walio wengi wa Misri wanataka sheria za nchi hiyo zibuniwe kutokana na mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press asilimia 62 ya wananchi hao wanaamini kwamba sheria za nchi hiyo zinapasa kuambatana na mafundisho ya Qur'ani na kwamba asilimia 27 wanaamini kuwa sheria zinazotungwa nchini humo zinapasa kwenda sambamba na thamani pamoja na misingi ya Uislamu.
Uchunguzi huo pia unaonyesha kuwa Wamisri ambao katika kipindi cha miaka 40 iliyopita walilazimika kutawaliwa na sheria zisizo za dini wana hamu ya kuona vyama vilivyo na mielekeo ya kidini vikishirikishwa serikalini. Asilimia 50 ya Wamisri wanasema kuwa kuna umuhimu na udharura wa kushirikishwa vyama hivyo serikalini ilihali asilimia 37 wanakikubali chama cha Ikhwanul Muslimeen ambacho ni chama kikubwa zaidi cha Kiislamu nchini humo. Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yalitangazwa rasmi siku ya Jumatatu, yaani miezi mitano kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge la Misri. 782226