Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Jumatano asubuhi, Mei 4, 2011, aliponana na maelfu ya walimu kutoka kona mbali mbali za Iran. Katika mkutano huo alisisitiza kwamba, jukumu kuu la kazi ya ualimu na usomeshaji ni kulea watu ndani ya misingi inayokubaliwa na harakati adhimu ya taifa la Iran chini ya kivuli cha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Ni kwa sababu hii ndio maana kazi ya usomeshaji na malezi inahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa kwa kuzingatia kigezo huru cha maendeleo ya Kiirani - Kiislamu ili matokeo yake yawe ni kupatikana watu waumini, wenye kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, watu wa heshima, mashujaa, wabunifu, wenye subira, wenye matumaini ya kupatikana mustakbali mwema, wenye akhlaki na maadili mazuri na ambao wakati wote wako tayari kungia kwenye medani mpya bila ya kuogopeshwa na hatari zake.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa pongezi zake pia kwa mnasaba wa siku ya kuadhimisha alipouawa shahidi Ayatullah Shahid Mutahhari ambayo ni siku ya walimu nchini Iran na kuongeza kwamba: Shahid Mutahhari alikuwa mtu mkubwa, mwenye busuri na muono wa mbali na aliyepambika kwa sifa za kuionea uchungu dini yake. Ameongeza kuwa: Mtu huyo mkubwa aliyepambika kwa sifa hizo maalumu alikuwa ni chimbuko la baraka nyingi katika upande wa elimu, utamaduni, taaluma na malezi na ndio maana mwishowe Mwenyezi Mungu alimpa zawadi wa kuuawa shahidi ili abakie hai kwa Mola wake, akiruzukiwa.
Aidha ametoa ufafanuzi kuhusu nafasi tukufu ya mwalimu na kusema: Mwalimu ni mtu ambaye jukumu la mustakbali wa nchi na malezi ya watu wakubwa, mujahidina katika njia ya haki na watu ambao wataiongoza nchi katika siku za usoni limo mikononi mwake, hivyo matabaka yote ya watu yanapaswa kujua thamani na umuhimu wa mwalimu na walinde heshima yake. Vile vile amesema, vyombo vya habari na viongozi nchini Iran nao wana jukumu kubwa la kutambulisha nafasi ya kweli ya mwalimu nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia suala la kuhitajika mabadiliko katika kazi ya usomeshaji na kufafanua zaidi kuhusu sababu za kutakiwa yawepo mabadiliko hayo akisema: Mfumo wa hivi sasa wa elimu nchini Iran inabidi ubadilikwe kwani ni wa kutoka nje na hauzingatii mahitaji na muktadha wa kiutamaduni wa taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Kitu cha lazima cha kufanikisha mabadiliko hayo ni kupatikana kigezo huru cha maendeleo ya Kiirani-Kiislamu ambapo kigezo hicho nacho inabidi kiwe ni cha kulea watu wenye viwango vinavyokubaliwa na utawala wa Jamhuri ya Kiislamu.
Amekumbusha kuwa: Kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kunyanyua juu bendera ya Uislamu na kujenga vizuri dunia na Akhera yake na kama inataka iwe msaidizi, shahidi na mtoa bishara njema kwa mataifa mengine, haina njia nyingine isipokuwa kujipinda kuwa na watu waumini, wenye kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, watu wa heshima, wabunifu, mashujaa, wapole, wenye vipaji vinavyochemka na ambao watakuwa tayari wakati wote kungia kwenye medani mpya bila ya kujali hatari zake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Jambo la lazima linalohitajika kwa ajili ya kulea watu wenye sifa hizo ni kutekeleza mambo yetu kwa mujibu wa maamrisho ya Uislamu na mafundisho ya Qur'ani Tukufu. Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia juu ya haja ya kujulikana misimamo inayopaswa kuchukuliwa kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika kazi ya ualimu na usomeshaji na kuongeza kwamba: Kuwa na mtazamo mpana na mpango mkubwa unaokusanya mambo yote na vile vile kuzingatia suala la kumfanya mwalimu kuwa mhimili, ni miongoni mwa masharti muhimu ya kuwezesha kupatikana mabadiliko hayo.
Ameongeza kuwa: Kiwango chochote cha uwekezaji kitakachotumika kwenye kuwekeza katika kazi ya ualimu na usomeshaji, bila ya shaka yoyote kitakuwa na matunda mazuri na mengi zaidi ikilinganishwa na uwekezaji katika sekta nyinginezo na inabidi watu wote waiangalie kazi ya ualimu na usomeshaji kwa jicho na mtazamo huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia pia kazi adhimu na ya kipekee iliyofanywa na taifa la Iran kwa uongozi wa busara ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) katika kipindi chote cha historia na kuongeza kuwa: Nchi ya Iran inahitaji kuwa na mfumo wa ualimu na usomeshaji ulio na hadhi ya taifa kama hili.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu vipengee vya harakati adhimu ya taifa la Iran akisema: Wakati mabeberu duniani wakiwa wametumia nguvu zao zote kupambana na matukufu ya Kiislamu na kibinaadamu, taifa la Iran limejitokeza likiwa na kaulimbiu mpya ya kuhuisha matukufu hayo na limeendelea peke yake na njia hiyo nzito hadi hivi sasa ambapo imefanikiwa kupata maendeleo na ushindi mkubwa katika jambo hilo.
Amesema harakati ya mwamko inayoshuhudiwa hivi sasa huko Magharibi, Asia na kaskazini mwa Afrika ni muendelezo wa harakati adhimu iliyoanzishwa na taifa la Iran na kusisitiza kuwa: Bila ya shaka yoyote harakati hii adhimu itakwenda hadi katika kitovu cha bara la Ulaya na kwamba wananchi wa mataifa ya Ulaya kuna siku watasimama dhidi ya wanasiasa na watawala wao ambao wamewafanya wananchi waburuzwe kibubusa na siasa za kiutamaduni na kiuchumi za Marekani na Wazayuni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kushuhudiwa mwamko huo katika nchi za bara la Ulaya ni jambo lisiloepukika na kuongeza kuwa: Mwamko unaoshuhudiwa hivi sasa umetokana na upana wa harakati adhimu ya taifa la Iran na kama tunataka kuona harakati hii inaendelea kwa kasi na nguvu zake hizi hizi, basi hatuna budi kutia nguvu mshikamano na umoja wetu sambamba na kuhakikisha kuwa vipaji vya watu wetu vinachanua zaidi na watu wanapata malezi bora ya muqawamah, imani, muono wa mbali, mwamko na taaluma ya hali ya juu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Bw. Haji Babai, Waziri wa Elimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba fupi na sambamba na kuashiria juu ya mipango na juhudi zilizofanywa na wizara yake katika kuleta mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa elimu nchini amesema: Siasa kuu za elimu nchini zimepasishwa katika Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Utawala wa Kiislamu nchini na kwamba falsafa ya malezi na usomeshaji nayo imo katika ajenda ya Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni.
786767