IQNA

Maafisa wa Saudia wakanusha madai ya BBC kuhusu maji ya Zamzam

19:34 - May 09, 2011
Habari ID: 2119455
Maafisa wa serikali ya Saudi Arabia wamekadhibisha ripoti ya televisheni ya BBC iliyodai kuwa maji ya Zamzam yamechafuka kwa kiwango kikubwa cha mada ya arseniki.
Mkuu wa jumuiya ya inayoshughulikia utaalamu wa masuala ya ardhi ya Saudia Zahir Nawwab amesema wataalamu wa kituo hicho hufanyia majaribio maji ya kisima cha Zamzam kila siku na hadi sasa hakuna ripoti yoyote inayothibitisha kwamba maji hayo yamechafuliwa na mada ya arseniki.
Awali kanali ya televisheni ya BBC ya Uingereza ilidai kuwa maji ya Zamzam yaliyoathiriwa mno na mada ya arseniki yanauzwa kinyume cha sheria kwa Wislamu katika maduka ya Uingereza.
BBC imesema japokuwa maji ya Zamzam hayauzwi katika nchi za nje lakini mahujaji wanaruhusiwa kutoka nje ya Saudi Arabia wakiwa na machupa ya maji hayo na kwamba machupa ya maji hayo yaliyofanyiwa uchunguzi na wataalamu yamekutwa na kiwango kikubwa cha mada ya arseniki.
Hata hivo Nawwab amesema kituo cha kugawa maji ya Zamzam cha Makka kinatumia viwango vya kimataifa katika kupima maji hayo na kwamba maji ya Zamzam yaliyotolewa na kituo hicho hayakuathiriwa na mada yoyote. Amesema yumkini maji hayo ya Zamzam yaliyokutwa London yaliathiriwa baada ya kufunguliwa machupa ya maji hayo.
Vilevile ubalozi wa Saudi Arabia mjini London umetoa taarifa ukisisitiza kuwa maji ya Zamzam ni safi na salama na kwamba majaribio ya kisayansi yamethibitisha kwamba kunywa maji hayo kuna faifa kwa afya ya mwanadamu.
Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani WHO linasema kuwa kiwango kinachoruhusiwa cha mada ya arseniki katika maji ya kunywa ni microgramu 10 katika kila lita moja ya maji na kwamba kiasi cha mada hiyo katika maji ya Zamzam kiko chini sana ya kiwango hicho. 788740


captcha