Baada ya njama za viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel za kukwamisha kutiwa saini maridhiano ya kitaifa ya Wapalestina kugonga mwamba na kutokuwa na natija, sasa viongozi wa utawala huo wa Kizayuni wanahaha huku na huko ambapo sasa wanawachukua mateka viongozi na wanaharakati wa makundi ya Kipalestina na hivyo kuzifanya njama zao kuchukua mkondo mpya.
Katika siku za hivi karibuni utawala wa Kizayuni ukiwa na lengo la kutoa pigo kwa maridhiano ya kitaifa ya Palestina umeongeza kasi ya kuwatia mbaroni viongozi na wanaharakati muhimu wa Harakati ya Jihadul Islami na Chama cha Hamas ukidhani kwamba, kwa njia hiyo asaa utaweza kuvuruga umoja uliopo hivi sasa baina ya Wapalestina. Duru za habari za kieneo, zinatathmini wimbi jipya la mashambulio na kamatakamata ya jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina kuwa lina lengo la kujaribu kutoa pigo kwa maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina yaliyotiwa saini hivi karibuni huko Misri baina ya Hamas na Fat'h. Hii inatokana na kuwa, Wazayuni na washirika wao wakubwa yaani Marekani hawajafurahishwa na hatua ya Wapalestina ya kufikia maridhiano ya kitaifa. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana utawala wa Kizayuni wa Israel ukishirikiana na Marekani ukaanza kutumia mkono wa chuma, siasa za mauaji na kuwateka viongozi na wanaharakati wa Kipalestina.
Katika kutekeleza siasa hizo za kinyama, makomando wa Israel wamevamia nyumba ya Majid Hassan mhadhiri wa Chuo Kikuu na mwanachama wa Hamas huko Ramallah na kisha kumchukua mateka na kumpeleka kusikojulikana. Aidha hivi karibuni Bassam Saadi mmoja wa wanachama wa Jihadul Islami naye amechukuliwa mateka akiwa pamoja na watu wengine wanne na kupelekwa kusikojulikana; hatua ambazo zinaashiria kuendelea siasa za kinyama za Wazayuni dhidi ya wanaharakati wa Kipalestina.
Ukweli wa mambo ni kuwa, hii sio mara ya kwanza kwa viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kutekeleza siasa za kuwafuta wanaharakati wa Kipalestina katika medani ya harakati huko Palestina; hatua ambazo bila shaka lengo lake ni kuvuruga hali ya amani na uthabiti katika ardhi hizo unazozikalia kwa mabavu. Siasa za Israel za kuwauwa viongozi na wanaharakti wa Kipalestina zilianza kutekelezwa kwa kasi kubwa mwaka 2006 baada ya utawala huo kushindwa katika njama zake za kutaka kuifuta Hamas katika uga wa siasa. Licha ya Wazayuni kutekeleza kwa nguvu zao zote njama dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, njama zake hizo zinaonekana kutokuwa na matunda yoyote hasa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa Palestina kwa harakati hiyo.
Siku zote nguzo za utawala wa Kizayuni wa Israel na kubakia hai utawala huo zimejengeka juu ya siasa za kufarakanisha, mauaji ya umati, kamatakamata na kuwatesa Wapalestina. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana hivi sasa baada ya kuondolewa pazia la hitilafu baina ya harakati za Fat'h na Hamas, viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wao wa Marekani kwa mara nyingine tena wameamua kutumia silaha ya vikwazo vya kifedha na kisiasa dhidi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kuwafuta viongozi wa harakati za mapambano ili kuzifanya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kukabiliwa na hali ya vurugu na machafuko.
788402