IQNA

Kongamano la ‘Mashia katika Karne za 20 na 21’ kufanyika London

17:15 - May 11, 2011
Habari ID: 2120220
Kituo cha Masomo ya Kiakademia ya Kishia mjini London kinapanga kuandaa kongamano lake la pili chini ya anwani ya ‘Mashia katika Karne za 20 na 21’ katika Kituo cha Kiislamu cha Imam Khoei kuanzia Oktoba 1-2 mwaka 2011.
Kongamano hilo linaandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo cha Masomo ya Afrika na Mashariki (SOAS).
Katika kipindi cha miongo kadhaa sasa ulimwengu wa Kishia umepewa umuhimu mkubwa kutokana na matukio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq.
Aidha kumeshuhudiwa ongezeko la Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mabara ya Amerika, Ulaya, Afrika na vilevile katika eneo la Ghuba ya Uajemi, Bara Hindi na Kusini Mashariki mwa Asia. Hayo yote yamepelekea kufanyika uchunguzi zaidi kuhusu jamii za Mashia duniani.
Kongamano hilo litajadili masuala ya kihistoria, kijamii, kisiasa, kidini, na kianthropolojia. Waandalizi wanawahimiza wasomi na wataalamu kuwasilisha mada kuhusu Mashia katika maeneo yaliyotajwa na kuashiria historia, chimbuko, changamoto za kisiasa na kidini zinazowakabili Mashia. Aidha wasomi wanaweza kuwasilisha mada kuhusu turathi za kiutamaduni za jamii za Mashia, mila na desturi zao na namna walivyoweza kuibua na kuunda tajriba zao za kipekee za kitaifa.
Vilevile wasomi wanaotaka kushiriki katika kongamano hilo wanaweza kuandika kuhusu mchango wa jamii za kishia katika uga wa kisiasa na nukta ambazo zimeendeleza au kuzuia ushiriki wao kisiasa. Aidha masuala kama vile elimu ya Mashia na namna wanafunzi wa Kishia walio katika madrasah wanajimudu katika mtaala wa kieneo na kitaifa yatajadiliwa katika kongamano hilo.
Vilevile kongamano hilo litajadili kuhusu Mashia waliohama katika maeneo mengine duniani na namna wanavyokabiliana na matukio ya kieneo na kimataifa.
Wanaokusudia kuwasilisha mada katika kongamano hilo wanaweza kutuma mukhtasari wa makala zao wa lugha ya Kiingereza. Mukhtasari wa makala usizidi maneno 300 na uwe katika muundo wa ‘word’. Siku ya mwisho ya kuwasilisha mukhtasari wa makala ni Mei 31 2011. Makala hizo zinapaswa kutumwa kwa anwani ya info@shiasearch.com.
789401
captcha