IQNA

Nchi na mashirika ya kimataifa yaunge mkono kubuniwa taifa la Palestina

19:17 - May 17, 2011
Habari ID: 2123592
Ikitoa taarifa kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa 63 wa kukumbukwa kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na kubuniwa rasmi utawala bandia wa Israel katika ardhi hizo, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC imetoa taarifa ikiyataka mataifa na mashirika ya kimataifa kuunga mkono suala la kubuniwa kwa taifa huru la Palesina katika mipaka ya mwaka 1967 mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu.
Taarifa hiyo imezisifu nchi ambazo tayari zimetambua rasmi taifa la Palestina na kuyataka mataifa ambayo hayajafanya hivyo kuchukua hatua hiyo muhimu ili kuondoa dhulma na uonevu ambao umekuwa ukitekelezwa kwa miaka mingi dhidi ya Wapalestina.
Taarifa hiyo imesisitiza kwamba OIC itaendelea kuwa kando ya wananchi wa Palestina katika kupigania haki na uhuru wao. Imesema ni miaka 63 sasa tokea Wapalestina wafukuzwe na utawala haramu wa Kizayuni kutoka kwenye ardhi zao za jadi na kulazimika kuishi kama wakimbizi katika nchi tofauti za duniani, jambo ambalo imesema linahesabiwa kuwa jinai na ubaguzi mkubwa zaidi wa kuwahi kutendeka katika karne ya 20.
Taarifa ya OIC imeendelea kusema kuwa inasikitisha kuona kwamba utawala haramu wa Israel unaendeleza vitendo vyake vya kujipanua na kubadili muundo wa kijamii katika ardhi za Wapalestina kwa kuendelea kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na kupora ardhi za Wapalestina ukiwemo mji mtukufu wa Quds bila kukabiliwa na upinzani wowote wa kimataifa. 792621
captcha