Abdu Rauf As-Shayyib, Kiongozi wa Harakati ya Uhuru ya Bahrain ambaye pia ni msemaji rasmi wa Muungano wa Februari 14 amesema kuwa mapambano ya wananchi wa Bahrain yataendelea hadi pale askari wote vamizi wa utawala wa kifalme wa Saudia watakapoondolewa nchini humo.
Amesema mapambano hayo yataongezeka katika siku za hivi karibuni. Amesema katika kipindi cha siku mbili zilizopita harakati za mapambano zimeongezeka dhidi ya utawala dhalimu wa Aal Khalifa kutokana na fatuwa za maulama na uungaji mkono unatolewa kutoka pande mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu.
Akiashiria kuondolewa kwa sheria ya hali ya hatari nchini humo As-Shayyib amesema kuwa utawala wa Aal Khalifa unatambua vyema kwamba kuwepo au kutokuwepo sheria hiyo hakuathiri kwa njia yoyote ile mapambano ya wananchi dhidi yake, na kwamba mapambano hayo yataendelea tu. Mwanasiasa huyo amesema kuwa kwa kufutilia mbali sheria hiyo utawala wa Manama unajaribu kuonyesha kwamba hali ya utulivu na amani imerejea nchini humo katika hali ambayo ukweli wa mambo nchini ni tofauti kabisa. Abdul Rauf amesisitiza mwishoni mwa matamshi yake juu ya udharura wa kuhukumiwa mahakamani watawala wote wa Bahrain waliohusika na jinai dhidi ya raia wa nchi hiyo na kuongeza kuwa mashtaka dhidi ya watawala hao tayari yamewasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC humo mjini Hague. 796258