Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Halmashauri ya Kimataifa ya Imam Hussein (as) ya mjini London.
Kwa mujibu wa gazeti la The News, Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan ni mmoja wa watu waliozungumza katika maadhimisho hayo ambayo yaliwashirikisha wafuasi wa dini tofauti. Zardari alisisitiza juu ya umuhimu wa wanadamu kufuata sira na maisha ya Bibi Fatma (as) akiwa ni nembo ya maadili bora kwa wanawake wote duniani.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa mwaliko wa Nadhir Ahmad, mwanachama wa kwanza katika Bunge la Wazee la Uingereza yaliwashirikisha wabunge wa mabunge yote mawili na viongozi wa dini tofauti zaidi ya 1000.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Lord John Alderdice wa chama cha European Liberal Democrat and Reform Party amesema kuwa kwa kufuata mfano wa maisha ya Bibi Fatma (as), wanawake wanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha uhusiano wa wafuasi wa dini za Nabii Ibrahim (as) bali katika jamii nzima ya mwanadamu.
Rubab Mahdi Mkuu wa Halmashauri ya Kimataifa ya Imam Hussein (as) amesema katika maadhimisho hayo kwamba kutambuliwa vyema shakhsia na maisha ya Bibi Fatma (as) kunaweza kuwasaidia wanawake katika kutatua matatizo yao mengi maishani.
Katika sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa binti huyo mtukufu wa Mtume (saw) Julian Band mwanachama wa Baraza la Kiislamu-Kikristo la Uingereza na Kuhani Mark Winer wa Hekalu la London Magharibi pia walizungumza katika hafla hiyo kuhusiana na masuala yanayofanana kati ya Uislamu, Ukristo na Uyahudi. 797634