IQNA

Raia wa kigeni umra kupindukia milioni nne

11:24 - May 26, 2011
Habari ID: 2128720
Idadi ya raia wa kigeni wanaofika katika ardhi tukufu za Makka na Madina kwa ajili ya ibada ya umra inazidi kuongezeka kila mwaka na inatazamiwa kufika milioni nne mwakani, amesema Waziri wa Hija wa Saudi Arabia Fouad Al Farsi.
Akizungumza Jumamosi wakati alipokutana na Gavana wa Makka Mwanamfalme Khaled al Faisal ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Hija, Al Farsi ametoa wito kwa taasisi zinazohusika na Hija kutoa huduma bora zaidi zinazowezekana kwa mahujaji.
Al Farsi amesema kuwa, 'Idadi ya wanaofanya ibada ya umra mwaka huu itakuwa laki saba zaidi ya mwaka jana. Ameongeza kuwa mji wa Makka tayari umejaa wafanyaziara kutoka maeneo mbalimbali ya dunia hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Pakistan, Misri, Uturuki, India, Malaysia, Indonesia na Bangladesh.
Naye mwanamfalme Khaled ametoa wito kwa watu wote wanaohusika kuendeleza juhudi za kuboresha huduma kwa wanaofanya ibada ya umra.
Serikali ya Saudia imetangaza kuwa pato la kila mwaka kutokana na wasafiri wa kigeni wanaoingia nchini humo litafika Riali za Kisaudia bilioni 80 ifikapo mwaka 2015.
Wakati huo huo wasafiri wanaoingia Saudia kwa ajili ya umra wametoa wito wa kuboreshwa huduma katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mfalme Abdulazizi mjini Jeddah.
Wageni wengi wanaopitia katika uwanja huo wanasema maafisa wa uhamiaji wanawadhalilisha jambo ambalo linaenda kinyume kabisa na maadili ya Kiislamu.
798174

captcha