Kituo cha Islam Today kimeripoti kuwa suala la ujenzi wa msikiti katika mji wa Milan limefanywa la kisiasa ambapo Meya wa mji huo Letizia Moratti ambaye aliwahi kuwa waziri wa Elimu ya Juu wa Italia anapinga vikali ujenzi huo.
Moratti anadai kuwa ujenzi wa msikiti katika mji wa Milan ambao ndio mji mkuu wa kiuchumi wa Italia, utawavutia Waislamu wengi katika mji huo, suala ambalo anadai litazusha hali ambayo haiwezi kudhibitiwa.
Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi pia amepinga vikali ujenzi wa msikiti katika mji wa Milan na amemuunga mkono kikamilifu meya wa mji huo.
Hata hivyo Askofu Mkuu w Italia Angelo Bagnasco ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kongresi ya Maaskofu wa nchi hiyo ametetea haki ya Waislamu ya kujenga msikiti mjini Milan.
Kutokana na hatua hiyo kundi kubwa zaidi la Waislamu wa Italia limetoa taarifa likimshukuru Askofu Mkuu na Jumuiya ya Maaskofu wa nchi hiyo na kusema uungaji mkono huo wa kujengwa sehemu rasmi kwa ajili ya ibada za Waislamu umethibitisha mshikamano wa kirafiki wa Wakristo waliowengi na dini nyinginezo. 799762