IQNA

Waislamu wa Bulgaria wataka kujengewa msikiti mpya katika mji mkuu

17:46 - May 29, 2011
Habari ID: 2130369
Imam wa msikiti pekee katika mji mkuu wa Bulgaria, Sofia ametaka Waislamu wa mji huo wajengewe msikiti mwingine kufuatia shambulio la hivi karibuni la waungaji mkono wa chama cha kibaguzi cha Ataka (Attack) dhidi ya waumini waliokuwa wakitekeleza ibada zao katika msikiti huo.
Imam huyo amesema viongozi wa mji huo wanapasa kuruhusu Waislamu kujenga msikiti mpya mkubwa katika mji huo ili kuzuia kukaririwa kwa kitendo kama hicho cha kibaguzi dhidi ya Waislamu. Amesema msikiti wa hivi sasa ni mdogo mno na kwamba hauwatoshi Waislamu kutekeleza ibada zao ipaswavyo. Amesema Waislamu wengi wanalazimika kuswalia kwenye barabara zilizo kando na msikiti huo, jambo linalopelekea kufungwa barabara hizo wakati wa ibada.
Imam wa msikiti wa Sofia amesema tokea sasa adhana itakuwa ikiadhiniwa kwa sauti ya chini ili kuepusha kukaririwa kwa shambulio jingine kama hilo dhidi ya Waislamu.
Akizungumzia suala hilo Hyussein Hafuzov Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu la Bulgaria amesema Waislamu wataendelea kutekeleza ibada zao katika msikiti huo ikiwemo swala ya Ijumaa kwa sababu wamehakikishiwa na viongozi wa mji huo kwamba watapewa ulinzi wa kutosha. Amesema licha ya kuwa msikiti wa Sofia una uwezo wa kubeba watu 1200 hadi 1500 lakini hivi sasa unabeba idadi kubwa zaidi ya hao na kwamba Waislamu wengi na hasa vijana hulazimika kuswali nje ya msikiti kutokana na uhaba wa nafasi kwenye msikiti huo.
Ameongeza kuwa Ijumaa iliyopita Waislamu waliswali kama kawaida katika msikiti huo bila kuhujumiwa na wabaguzi wa rangi. 800148
captcha