Kongamano hilo linahudhuriwa na wanafikra kutoka zaidi ya nchi 20 zikiwemo Iraq, Uingereza, Ujerumani, Indonesia, Russia, Qatar, Uturuki, Misri na Ufaransa. Mada kuu ya kongamano hilo la kimataifa ni kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika na taathira zake katika mfumo wa kimataifa.
Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba harakati za wananchi zilizoanzia kaskazini mwa Afrika hadi Mashariki ya Kati sasa zimekuwa kigezo cha mwamko wa Kiislamu na kusimama kidete mbele ya ubeberu wa kimataifa. Mabadiliko hayo yametokana na itikadi zilizojuu ya masuala ya kisiasa na kimadhehebu ambazo ni suala la kupambana na dhulma na kueneza uadilifu.
Harakati ya mwamko wa Kiislamu iliyoanza sambamba na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, tukio ambalo halikuwa na mfano wake katika miaka ya mwishoni mwa karne ya 20, sasa inatoa bishara njema za mabadiliko ya kimsingi katika medani ya kieneo na kimataifa katika milenia ya tatu. Hapana shaka pia kwamba harakati hii kubwa itakuwa na taathira katika mustakbali wa mataifa ya maeneo hayo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndiyo maana Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla zinafanya jitihada za kujaribu kudhibiti harakati hizo za wananchi kupitia njia ya kupotosha malengo yake na kuanzisha vita vya ndani kama inavyoshuhudiwa hivi sasa katika nchi za Libya na Yemen. Nchi hizo za kikoloni hususan Marekani zinaituhumu Iran kuwa inaingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine kama Bahrain ili kwa njia hiyo ziweze kubadili mwenendo wa harakati ya mwamko wa Kiislamu.
Hapa linajitokeza swali kwamba, ni nchi gani iliyoanzisha vituo vya kijeshi katika eneo hili la Mashariki ya Kati kwa ajili ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi za eneo hili?
Nchi za Magharibi zinaendeleza mashambulizi makali dhidi ya utawala wa Libya wakati ambapo majeshi ya NATO na ya Uingereza yanatoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa Saudi Arabia na Imarati kwa ajili ya kukandamiza wananchi wa Bahrain wanaodai haki zao za kisheria. Saudi Arabia na Imarati zimetuma zaidi ya askari jeshi elfu moja huko Bahrain kwa ajili ya kuzima harakati za kidemokrasia za kudai haki zao za kisheria. Hata hivyo na licha ya siasa hizo za kishetani lakini harakati ya mwamko wa Kiislamu ambayo imepewa jina la "Tsunami ya Kisiasa" inashika kasi zaidi.
Wanadharia wengi wanasema kuwa mwamko wa sasa wa Kiislamu katika nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika umekuwa changamoto kubwa inayovuruga usingizi wa nchi za kibeberu zilizozoea kupora utajiri na maliasili ya maeneo hayo kwa kuwaunga mkono watawala madikteta ambao sasa viti vyao vinatokota moto.
801974