IQNA

Waziri wa Ufaransa afutiwa tuhuma ya dharau dhidi ya Waislamu

14:25 - June 11, 2011
Habari ID: 2136023
Mahakama ya Jamhuri ya Ufaransa CJR siku ya Ijumaa ilifutilia mbali tuhuma ya dharau na kuwavunjia heshima Waislamu pamoja na kutoa matamshi ya kibaguzi iliyokuwa ikimkabili Claude Gueant Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo.
Hii ni katika hali ambayo suala la ubaguzi na siasa za kibaguzi zinazotekelezwa na serikali ya Ufaransa dhidi ya jamii za wachache nchini humo pia zimekosolewa na Umoja wa Mataifa.
Kwa hatua ya mahakama hiyo Waziri huyo sasa hatafuatiliwa tena na vyombo vya sheria vya nchi hiyo kutokana na mashtaka yaliyowasilishwa mahakamani dhidi yake na jumuiya inayopinga ubaguzi ya Ufaransa kutokana na matamshi ya kibaguzi aliyotoa hivi karibuni dhidi ya Waislamu.
Waziri huyo alifikishwa mahakamani kutokana na matamshi yake aliyotoa dhidi ya Waislamu kwa kudai kwamba idadi yao inaongezeka kwa kasi kubwa nchini humo na kutaka mwenendo huo usimamishwe mara moja.
Jumuiya ya kupambana na ubaguzi nchini Ufaransa imekosoa uamuzi wa mahakama hiyo na kusema kuwa inatiwa wasiwasi kutokana na kulindwa wanasiasa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu mashtaka yanayowakabili. 806169
captcha