IQNA

Njama za Utawala wa Kizayuni dhidi ya Quds Tukufu zalaaniwa

14:23 - June 26, 2011
Habari ID: 2144438
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC amelaani hujuma inayoendelea ya utawala wa Kizayuni dhidi ya turathi za Kiislamu.
Prof. Ekmeleddin İhsanoğlu kupitia taarifa iliyotolewa na makao makuu ya OIC mjini Jeddah amelaani hujuma ya Israel dhidi ya turathi za Kiislamu za Kasri za Khalifa za Kiummawi zilizo kusini mwa Msikiti wa Al Aqsa. Utawala wa Kizayuni unataka kuziweka turathi hizo za Kiislamu katika kile kinachotajwa kuwa Mabustani ya Torati katika fremu ya mpango wa kuuyahudisha mji wa Quds. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ameitaja hatua hiyo ya utawala unaokalia Quds kwa mabavu kuwa ni hujuma dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa. Ameutaja uchimbuaji wote unaofanya na Israel katika Baitul Muqqadas kuwa ni kuwa ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na mikataba ya Geneva.
Onyo la Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu linakuja kufuatia kushadidi hujuma haribifu za utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa. Kushtadi hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa ni jambo linaloashiria kuingia katika awamu ya hatari njama za utawala huu ghasibu dhidi ya Msikiti wa al Aqsa.
Hivi karibuni duru za Kipalestina zilifichua njama za Utawala wa Kizayuni za kuuharibu kabisa mji wa Baitul Muqqadas na mahala pake kujenga mji mpya wa Kizayuni. Utawala haramu wa Israel unataka kudhibiti kikamilifu mji wa Baitul Muqqadas na kwa hivyo utawala huo ghasibu umeshadidisha hatua zake haribufu dhidi ya maeneo ya Kipalestina na Kiislamu katika mji huu. Kupitia hatua zake haribifu utawala wa Kizayuni unataka kuupa mji wa Quds sura za Kizayuni. Mji wa Baitul Muqqadas au Quds unapewa umuhimu katika sera za kijitanua utawala haramu wa Israel. Ni kwa sababu hii ndio utawala huo wa Kizayuni mnamo mwaka 1948 uliteka na kukalia kwa mabavu Quds Magharibi na mwaka 1967 ukakalia kwa mabavu Quds Mashariki.
Utawala wa Kizayuni sasa ili kukalia kwa mabavu kikamilifu Baitul Muqqadas umezidisha sera zake za kijipanua katika mji huu. Utawala wa Kizayuni pia unafuatilia sera za kubadilisha muundo wa idadi ya watu na kijiografia katika maeneo ya Kipalestina. NI katika fremu hii ndio tunashuhudia hatua haribifu za utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Kipalestina hasa Baitul Muqaddas. Hujuma haribifu ya utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya Palestina ni ukiukwaji wa wazi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Geneva, utawala wa Kizayuni umeonywa kutoingia na kuteka maeneo ya Wapalestina. Kwa hivyo hujuma za Wazayuni zimewatia wasiwasi walimwengu hasa nchi za Kiislamu. Ni kwa sababu hii ndio Wapalestina na nchi za Kiislamu zinataka jamii ya kimataifa hasa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Umoja wa Mataifa uchukue hatua kali dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Kuzembea katika kukabiliana na hatua haribifu za utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina hasa Quds Tukufu na kutosheka tu kulaani kwa maneno ni mambo ambayo yanaupa kiburi zaidi utawala wa Kizayuni kuendeleza ushetani wake wa kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu.

814676
captcha