IQNA

Kongamano la Kimataifa la 'Qur'ani, Kitabu cha Mwamko' lafanyika Tehran

16:04 - August 15, 2011
Habari ID: 2171331
Kongamano la kimataifa la 'Qur'ani, Kitabu cha Mwamko' lilifanyika jana jioni kandokando ya Maonyesho ya 19 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yanayoendelea hapa mjini Tehran.
Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu alihutubia kongamano hilo akieleza nafasi ya Qur'ani katika kuuamsha umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa masuala yote yanayohusiana na mwamko wa Kiislamu na udharura wake vimezungumziwa katika aya za Qur'ani Tukufu.
Ayatullah Taskhiri amesema kuwa Qur'ani ni kitabu cha milele cha Mwenyezi Mungu kinachokusanya mambo yote na kila mtu anaweza kukidhi mahitaji yake kwa kurejea kwenye aya za kitabu hicho.
Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu la Iran Muhammad Baqir Khurramshad pia amehutubia kongamano hilo la kimataifa akisema kuwa tunapozungumzia mwamko tunamaanisha kwamba sehemu ya umma wa Kiislamu imelala na sasa imo katika hali ya kuamka kutokana na kurejea kwenye mafundisho ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa mghafala na usingizi huo huupata umma wakati Waislamu wanapopatwa na udhaifu na kuporomoka katika masuala ya utamaduni na ustaarabu.
Mkutano huo wa kimataifa wa Mwamko wa Kiislamu unahudhuriwa na wasomi, wanafikra na wanaharakati wa masuala ya Qur'ani kutoka nchi mbalimbali. 843265

captcha