IQNA

Baraza la Kitaifa la Mapinduzi laundwa Yemen

12:17 - August 20, 2011
Habari ID: 2173768
Vyama vya upinzani vinavyoipinga serikali ya Rais Abdullah Swaleh wa Yemen vimeunda Baraza la Kitaifa la Mapinduzi. Baraza hilo lililobuniwa siku ya Jumatano tarehe 17 Agosti ni hatua muhimu katika juhudi za kubuni serikali huru nchini humo.
Baraza hilo ambalo litakuwa na wajumbe 143 kutoka vyama vyote vya upinzani vya Yemen litachukuliwa kuwa mwakilishi pekee na rasmi wa wananchi wa Yemen na litakuwa na jukumu la kufanya juhudi za kutambuliwa rasmi kieneo na kimataifa.
Wanachama wa baraza hilo wanatazamiwa kukutana hivi karibuni ili kumchagua mkuu wake pamoja na wanachama 20 ambao watasimamia masuala ya uandamizi na uendeshaji wa harakati ya mapinduzi dhidi ya Rais Abdullah Swaleh.
Baraza hilo limeundwa masaa machache tu baada ya Abdullah Swaleh aliye nchini Saudi Arabia kwa matibabu kutangaza kuwa ana nia ya kurejea Yemen hivi karibuni na kwamba ataondoka madaraka tu kupitia uchaguzi na wala sio kuondolewa kwa nguvu. 846123
captcha