Hapo jana katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani mamilioni ya Wairani walijitokeza mabarabarani nchi nzima kulaani dhulma inayofanywa na Israel dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina na kuunga mkono muqawama dhidi ya Wazayuni maghasibu.
Wananchi wa Bahrain walijitokeza kwa wingi kwenye maandamano ya siku ya Quds licha ya serikali ya Manama kupiga marufuku maandamano hayo, huku wananchi wa Misri wakiandamana kwa hasira mbele ya ubalozi wa Tel Aviv mjini Cairo.
Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds yalifanyika pia nchini Yemen, Pakistan, Uturuki, Lebanon, Iraq, Afghanistan, baadhi ya miji ya Saudi Arabia, Moscow, Pretoria na miji mbalimbali duniani.
Inafaa kukumbusha kuwa Imam Khomeini MA Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran miongo mitatu iliyopita aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa Waislamu katika kuunga mkono haki za Waislamu wa Palestina.
849910