Katika taarifa iliyotolewa baada ya kumalizika kikao chake hapa Tehran, baraza hilo la wanazuoni wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa mapinduzi ya Kiislamu limesema kuwasaidia watu wanaokumbwa na njaa huko Somalia ni wajibu wa Kiislamu na kibinaadamu. Baraza hilo limewashukuru wananchi wa Iran ambao wametoa misaada kwa Wasomali na kutoa wito wa kuendelea utoaji misaada hadi wanaokumbwa na njaa warejee katika hali ya kawaida.
Kwingineko katika taarifa yake, baraza hilo limesisitiza kuwa mapambano ni haki ya kisheria ya Wapalestina na kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel ni bandia. Wanazuoni hao wametoa wito kwa Wapalestina kuungana katika harakati zao za kupigania ukombozi. Wakati huo huo Baraza hilo limesema mwamko wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni kinyume cha matakwa ya madola ya kibeberu na limetoa wito kwa wananchi wanamapinduzi katika eneo hilo kuchukua tahadhari ili madola ya kigeni hasa Marekani na Utawala wa Kizayuni yasiteke mapinduzi hayo ya wananchi. Aidha baraza hilo limelaani vikali ukandamizwaji wananchi unaofanywa na utawala wa Kifalme nchini Bahrain. 855386