IQNA

Utawala wa Bahrain wafanya njama ya kuwafukuza Mashia nchini

18:40 - September 14, 2011
Habari ID: 2187108
Mmoja wa washauri wa zamani wa utawala wa kifalme wa Bahrain amefichua kwamba utawala huo umebuni kikosi maalumu cha askari usalama kwa ajili ya kukandamiza na kuwalazimisha Mashia waliowengi wa nchi hiyo kukimbia na kuhamia kwingineko kwa maslahi ya utawala huo.
Njama hiyo inapangwa ili kubadili muundo wa kijamii na kimadhehebu wa hivi sasa unaotawala nchini Bahrain ambao ni kwa maslahi ya jamii ya waliowengi ya Mashia. Utawala wa Manama unadhani kwamba utaweza kujidhaminia usalama kwa kuwafukuza Mashia nchini humo. Kwa mujibu wa kauli ya Swalah al-Bandar, mshauri wa zamani wa Wizara ya Masuala ya Baraza la Mawaziri ya Bahrain, watawala wa sasa wa Manama wanaamini kwamba usalama wao utadhaminiwa tu pale jamii ya Mashia itakapopunguzwa na kufanywa kuwa ya wachache. Kwa mujibu wa ripoti ya al-Bandar, Mashia wanapaswa kupunguzwa na kuwa kati ya asilimia 20 hadi 30 ya jamii nzima ya nchi hiyo. Amesema ukoo wa kifalme wa Aal Khalifa umelitaka bunge kujiepusha kujadili suala la idadi ya raia wa Bahrain kwenye vikao vya bunge kwa sababu tayari serikali imewapa uraia wa Bahrain raia wa Kisuni 15,000 kutoka nchi za Misri, Jordan, Kuwait na Morocco ili kufikia lengo lililotajwa dhidi ya Mashia. Ripoti hiyo inasema kuwa mbinu nyingine inayotumiwa na utawala wa Aal Khalifa kupunguza idadi ya Mashia nchini, ni kuwapa kazi raia wa kigeni ndani ya nchi na kuwatafutia Mashia nafasi kama hizo nje ya nchi. Amesema kuzusha mifarakano ya kimadhehebu, kupunguza idadi ya Mashia kwenye nafasi nyeti wizarani na idara za serikali, mashirika ya mambo ya kheri, Mashirika binafsi na kwa ujumla katika sekta ya uchumi, ni njama nyingine zinazotekelezwa na ufalme huo dhidi ya raia wake wa Kishia. 860410
captcha