IQNA

Ikhwanul Muslimin ya Jordan yamuonya mfalme wa nchi hiyo

14:50 - September 19, 2011
Habari ID: 2189866
Mmoja wa viongozi wa mrengo wa Kiislamu wa Amal, ambalo ni tawi la kisiasa la Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Jordan amemtahadharisha Mfalme Abdallah wa nchi hiyo dhidi ya kuchukua hatua zozote za kijeshi nchini Libya.
Akibainisha suala hilo, Zaki Bani Arshid, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Amal ambacho ni moja ya vyama muhimu vya upinzani nchini Jordan amesisitiza kwamba mafunzo yoyote ya kijeshi au polisi yatakayotolewa na jeshi la nchi hiyo kwa askari wa Libya kwa ushirikiano wa Marekani au Nato ni kinyume na matakwa ya Wajordan kwa sababu wanapinga vikali ubeberu wa Marekani na nchi za Magharibi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Amesema ushirikiano wa Jordan na Marekani katika kueneza vita dhidi ya umma wa Kiislamu ni tishio kwa usalama wa kitaifa wa Jordan. Amesema hii inatokana na ukweli kwamba, askari wa Jordan watakapoonekana kuwa wanashirikiana na Marekani dhidi ya Waislamu wenzao wa Libya, watachukuliwa kuwa ni washirika wa maadui wa Waislamu na hivyo kuhatarisha usalama wao na wa taifa zima la Jordan.
Awali Nassir Jauda, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan alitangaza kuwa nchi hiyo ilikuwa tayari kutuma askari wake nchini Libya ili kushirikiana na Marekani katika kutoa mafunzo ya kijeshi na polisi kwa askari wa nchi hiyo kwa lengo la kuimarisha usalama na uthabiti wake.
Mfalme Abdallah II wa Jordan alitangaza katika kikao kilichofanyika hivi karibuni mjini Paris Ufaransa kwamba nchi yake iko tayari kutuma askari nchini Libya ili kusaidia kutoa mafunzo hayo kwa askari wa Libya. 863494
captcha