IQNA

Kikao cha UN kuhusu Palestina kimemalizika bila ya natija

21:47 - September 27, 2011
Habari ID: 2194576
Ripoti zinaarifu kuwa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika usiku wa kuamkia leo huko New York ili kuchunguza ombi la Wapalestina la kutaka kuundwa nchi huru ya Palestina na nchi hiyo kupatiwa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa kilimalizika bila ya natija yoyote ya maana.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao hicho kilichohudhuriwa na nchi tano wanachama wa kudumu yaani Ufaransa, Uingereza, Marekani, Uchina na Russia na nchi nyingine wanachama wasio wa kudumu yaani Lebanon, Brazil, India, Afrika Kusini, Ujerumani, Bosnia Herzegovina, Gabon, Colombia, Nigeria na Ureno. Nawaf Salam mwakilishi wa kudumu wa Lebanon na Mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa alisema mwishoni mwa kikao cha baraza hilo kuwa, Baraza la Usalama Jumatano wiki hii pia litakuwa na kikao kingine kuhusiana na ombi la Wapalestina. Ameongeza kuwa iwapo Baraza la Usalama litapasisha uanachama wa Palestina katika umoja huo, suala hilo litawasilishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kupigiwa kura ya mwisho.
Hii ni katika hali ambayo, Marekani imetangaza wazi wazi kwamba, italipigia kura ya turufu ombi hilo la Wapalestina. Marekani inatishia kulipigia kura ya veto katika Baraza la Usalama ombi hilo lililowasilishwa na Wapalestina juu ya kuunda nchi ya Palestina katika hali ambayo, tukitupia jicho utendaji wa Marekani kuhusiana na mgogoro wa Palestina, tunaona chuki, uadui na uhasama mkubwa wa nchi hiyo dhidi ya wananchi wa Palestina. Sambamba na hayo, Marekani imepinga hata suala la kukosolewa tu na kulaaniwa Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.
Kwa kuzingatia hayo yote, tunaweza kufikia natija kwamba hakuna shaka yoyoye kuwa Marekani haitasita kutumia kura isiyo ya kiadilifu ya veto au njama nyingine yoyote dhidi ya wananchi wa Palestina. Uungaji mkono huo wa pande zote wa Marekani kwa utawala bandia wa Israel umekosolewa vikali na fikra za waliowengi duniani. Kwa msingi huo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kutokana na upinzani mkali wa fikra za walimwengu kwa misimamo ya kiupendelea ya Marekani kwa Israel yumkini Washington ikajaribu kutumia njama nyingine kama ya kurefusha mwenendo wa kushughulikia ombi la Wapalestina na hata kukwamisha uchukuaji wa maamumuzi kwa kupindishapindisha vikao vya Baraza la Usalama na hatimaye kuwanyima Wapalestina haki ya kuwa na nchi huru. 868183



captcha