IQNA

Wazayuni wakasirishwa na hotuba ya Imam Khamenei katika mkutano wa Tehran

10:56 - October 02, 2011
Habari ID: 2197084
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameelezea kuchukizwa mno na hotuba iliyotolewa jana na Imam Ayatullah Ali Khamenei katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Mapambano ya Intifadha ya taifa la Palesina.
Benjamin Netanyahu amedai kuwa mkutano huo unaimarisha zaidi nafasi ya Israel!
Akionyesha radiamali yake kuhusu hotuba zinazotolewa katika mkutano huo wa kimataifa ambazo zinasisitiza kuwa utawala ghasibu wa Israel umetengwa kimataifa, Netanyahu amedai kwamba hotuba hizo zinaimarisha nafasi ya serikali ya Israel.
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amesema: "Serikali yangu ina msimamo thabiti ambao ni kulinda amani ya ndani na kufanya juhudi za kutambuliwa rasmi nchi ya Mayahudi wote."
Benjamini Netanhayu amedai pia kwamba malengo ya washiriki katika mkutano wa Tehran ni kuangamiza Israel na yanazidisha haja ya kulindwa Israel na kutambuliwa rasmi kama nchi ya Kiyahudi.
Mapema jana Imam Ali Khamenei alifungua mkutano wa kimataifa wa kuunga mkono mapambano ya Intifadha ya taifa la Palestina na kusisitiza kuwa mpango wowote unaokusudia kuigawa Palestina haukubaliki.
Ayatullah Khamenei alisema kuwa utawala bandia wa Israel ni sime ya nchi za Magharibi katika mbavu za umma wa Kiislamu na kwamba dola hilo bandia limekuwa kambi ya kijeshi, kisiasa na kiusalama ya ubeberu katika eneo nyeti zaidi la ulimwengu wa Kiislamu kwa shabaha ya kukabiliana na Uislamu na Waislamu. 871353



captcha