Taqrib au kwa ibara nyingine ukurubishaji pamoja wa madhehebu ya Kiislamu ni njia bora zaidi ya kuuondoa umma wa Kiislamu katika giza ambalo umekuwa ukiishi ndani kwa miaka mingi, jambo ambalo linaandaa uwanja mzuri wa kufikiwa maendeleo ya umma wa Kiislamu.
Jambo hilo pia linaandaa uwanja wa kujikwamua umma wa Kiislamu kutoka kwenye minyororo ya maadui wa Uislamu. Ni wazi kuwa kama jambo hilo halitathibiti, maadui wa Uislamu wataendelea kutazama utajiri wa umma wa Kiislamu kwa jicho la tamaa na kuendelea kufanya njama za kuwadhuru Waislamu ili kunufaika na utajiri huo bila kukabiliwa na kikwazo.
Huo ndio ujumbe muhimu ulioakisiwa kwenye taarifa ya mwisho ya kikao cha kimataifa cha maulamaa, wanafikra na wasomi wa Kiislamu kilichomalizika jana Jumamosi huko London mji mkuu wa Uingereza. Washiriki wa kikao hicho wamesema kuwa juhudi za kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu ambazo zimekuwa zikiendelea kwa miaka kadhaa sasa, zina nafasi muhimu katika kuainisha mustakbali wa umma wa Kiislamu.
Taarifa ya mwisho ya washiriki wa kikao cha London imesema kuwa wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu wana jukumu zito la kueneza mafundisho ya Kiislamu na kuwabainishia wafuasi wao hatari kubwa inayoukabili umma wa Kiislamu hasa kutoka madola makubwa ya Magharibi. Imewataka wanafikra na wanazuoni wa Kiislamu kujiepusha na masuala yanayowatenganisha Waislamu na kujishughulisha na yale yanayowaunganisha kwa lengo la kukabiliana na hatari zinazoweza kuudhuru umma wa Kiislamu.
Washiriki wa kikao hicho wamewataka Waislamu kuzingatia malengo ya kuleta mwamko katika nchi za Kiislamu na kutohadaika na ahadi za uongo zinazotolewa na nchi za Magharibi kwa lengo la kuugonganisha umma wa Kiislamu. 871496