Imam wa Ijumaa wa mjini Awamiya nchini Saudi Arabia, ameashiria matukio ya ghasia za hivi karibuni nchini humo na kusema kuwa watawala wa nchi hiyo wanatekeleza njama hatari dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Akizungumza katika Swala ya Ijumaa hapo jana, Ayatullah Sheikh Namr Baqir, Aal Namr amewakosoa vikali watawala wa serikali ya Riyadh kuhusiana na matukio ya hivi karibuni katika miji ya Mashia na kusema kuwa madai yao kuwa chanzo cha ghasia hizo ni nchi moja ya kigeni hayana msingi wowote. Akizungumza katika Msikiti wa Imam Hussein (as) katika mji wa Awamiya Ayatullah Namr amevunjilia mbali madai ya hivi karibuni ya watawala wa Saudia kuhusiana na kuwepo mkono wa nje katika matukio hayo na kusema kuwa watawala hao ndio wanaopanga na kutekeleza njama za kiuadui dhidi ya Mashia.
Ayatullah Aal Namr amewataka wanazuoni na wasomi wa nchi hiyo kuwa waangalifu na kujiepusha kutumbukia kwenye mtego uliowekwa na watawala hao kwa kutojiingiza moja kwa moja kwenye vitendo vya ghasia. 875403