IQNA

Wikileaks yafichua jinsi Saddam alivyoshambulia Haram ya Imam Hussein AS

17:45 - October 09, 2011
Habari ID: 2201753
Mtandao wa Wikileaks umefichua habari za ndani za jinsi dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein alivyoshambulia Haram tukufu ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW Imam Hussein bin Ali AS katika mji mtakatifu wa Karbala na kuua Waislamu waliokuwa wamekwenda hapo kwa ajili ya ibada.
Waraka uliochapishwa na Wikileaks kuhusu jinai za utawala wa Saddam Hussein umesema kuwa mwaka 1991 dikteta huyo aliitisha kikao kilichojumuisha wanaye mawili Uday na Qusay na mkwe wake Hussein Kamil katika ikulu ya Sujud kwa ajili ya kupanga shambulizi dhidi ya Haram ya Imam Hussein AS mjini Karbala na Waislamu waliokwenda kufanya ziara katika eneo hilo takatifu.
Waraka huo wa Wikileaks unasema kuwa Uday mwana wa Saddam alimuamuru Kamil Hussein ashambulie maeneo yote ya Karbala bila kushauriana na baba yake yaani Saddam, lakini Kamili alikwenda kushauriana na Saddam kisha dikteta huyo akamtaka ashambulie minara na kuba za Haram ya Imam Hussein AS na kukata vichwa vya watu waliokuwa wakifanya ziara.
Wikileaks imeripot kuwa: Kamil Hussein alimtaka Jenerali Qais Hamza Aboud ashambulie minara na kuba za Haram ya Imam Hussein na Amirul Muuminina Imam Ali bin Abi Twalib AS na Saddam Hussein akamtaka awashambulie watu wote waliokenda kufanya ziara katika maeneo hayo na kukata vichwa vya watu watakaokamatwa na askari usalama.
Waraka wa Wikileaks unasema kuwa Kamil Hussein alishambulia kuba la Haram ya Imam Hussein AS kwa kutumia kifaru cha gadi makhsusi ya rais na baada ya kutimiza ukatili alioamrishwa kufanya alipeleka ripoti ya shambulizi hilo kwa Saddam Hussein ambaye aliahidi ya kumtunza.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa mwaka 1991 serikali ya kidikteta ya Saddam Hussein ilishambulia miji mitakatifu ya Najaf na Karbala kwa shabaha ya kuzima harakati za wananchi katika maeneo hayo na kuua wakazi wake kwa umati. Jeshi la Saddam pia lililenga kuba na milango ya Haram tukufu za Imam Ali bin Abi Twalib, Imam Hussein na Abul Fadhl Abbad AS.
Siku hiyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei alitangaza maombolezo ya kitaifa kote nchini. 876332

captcha