Kwa mujibu wa tovuti ya televisheni ya al-Alam, Wamisri wengi walikusanyika jana usiku mjini Cairo na kupiga nara za kulaani mauaji ya hivi karibuni mjini humo na kutaka wanajeshi wote waliohusika katika ghasia na mauaji hayo kufikishwa mahakamani.
Watu 25 waliuawa na wengine 300 kujeruhiwa katika mapigano yaliyojiri hivi karibuni kati ya Wakristo wa Kikopti na askari usalama wa Misri. Waandamanaji wamesisitiza kwamba hayo hayakuwa mapigano ya kidini bali yalikuwa mauaji ya umati yaliyotekelezwa na wanajeshi na kumtaka mkuu wa Baraza la Kijeshi linaloongoza nchi hiyo kwa muda ajiuzulu. Vilevile wamemtaka Usama Heikal, Waziri wa Habari wa nchi hiyo pia ajiuzulu wakimtuhumu kuwa aliruhusu televisheni ya taifa kuripoti matukio hayo kwa upendeleo fulani na kwa madhumuni ya kuzusha fitina miongoni mwa Wamisri.
Baadhi ya watu walioshuhudia matukio hayo wanasema kuwa wanajeshi waliwalenga raia kwa risasi moja kwa moja na na hata kuwakanyaga wengine kwa magari yao ya kijeshi.
Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita jeshi lilikanusha habari kwamba linatumia nguvu dhidi ya raia. 879779